1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia 7 wa kigeni wauwawa Nigeria

Tsuma Carolyne11 Machi 2013

Italia na Ugiriki zimethibitisha kuwa raia saba wa kigeni waliotekwa nyara kutoka kampuni moja ya ujenzi mwezi uliopita na kundi haramu la Ansaru nchini Nigeria wameuwawa.

https://p.dw.com/p/17uqm
Kundi la kigaidi la Anasaru lawauwa raia wa kigeni Nigeria
Kundi la kigaidi la Anasaru lawauwa raia wa kigeni NigeriaPicha: picture alliance/AP Photo

Kundi lililo na mafungamano na mtandao wa al-Qaida, Ansaru, siku ya Jumamosi lilitangaza kuwa liliwauwa raia saba kutoka mataifa ya kigeni waliowateka nyara tarehe 7 mwezi uliopita katika jimbo liliko kaskazini la Bauchi kwa sababu ya majaribio ya majeshi ya Nigeria na Uingereza kuwaokoa.

Kundi hilo lilichapisha picha zinazoonyesha miili ya raia wa Uingereza, Italia, Ugiriki na wafanyakazi wanne wa kutoka Lebanon waliotekwa nyara kutoka majengo ya  kampuni ya Kilebanoni.

Nigeria bado haijathibitisha vifo

Hadi jana, mataifa ambayo raia wake walitekwa yalikuwa hayajaweza kuthibitisha mauaji hayo. Italia na Ugiriki zimekanusha kuwa kulikuwa na jaribio lolote la  serikali zao kuwaokoa mateka. Serikali ya  Nigeria nayo haijaweza kuthibitisha mauaji hayo kufikia sasa.

Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia inasema kuwa wanaamini kuwa taarifa za kijasusi walizozipokea pamoja na mataifa mengine husika, zinathibitisha kuwa habari za kuuwawa kwa mateka hao ni za kweli na kuongeza kuwa rais wa Italia ametuma risala za rambirambi kwa familia ya raia wa Italia aliyeuwawa.

Waziri wa mambo ya nje wa Italia Giulio Terzi
Waziri wa mambo ya nje wa Italia Giulio TerziPicha: Reuters

Afisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imetoa jina la raia wake aliyeuawa kama Brendan Vaughan. Taarifa za kijasusi kutoka Nigeria zinasema raia wa Italia, Silvano Trevisan, alikuwa na matatizo ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo.

Hali ya usalama imekuwa mashakani katika kampuni za mafuta na miundo mbinu katika kanda hiyo ya magharibi mwa Afrika tangu wanamgambo wanaofunagamana na mtandao wa al-Qaida kuvamia kiwanda kimoja cha gesi nchini Algeria mwezi Januari na kuwauwa karibu raia 37 wa kigeni katika jaribio la jeshi la Algeria kuwaokoa.

Hatari imeongezeka zaidi katika mataifa ya magharibi na kaskazini mwa Afrika tangu Ufaransa itume majeshi yake nchini Mali kudhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo iliyo ngome ya waasi wenye mafungamano na al-Qaida.

Jeshi la Ufaransa nchini Mali
Jeshi la Ufaransa nchini MaliPicha: dapd

Makundi ya kigaidi yazidi kuwa tisho

Makundi ya kigaidi pia yameenea kaskazini na eneo la kati mwa Nigeria ambako kuna utajiri mkubwa wa mafuta na kuwa tisho kwa usalama  wa taifa hilo. Utekaji nyara hasa unaolenga raia wa kigeni si jambo geni katika eneo hilo kwa miaka mingi na makundi yanayoteka nyara hudai kulipwa kitita cha fedha kabla ya kuwaachilia huru mateka wao, lakini katika siku za hivi karibuni mkondo umebadilika na matokeo yake ni vifo.

Kundi hilo la Ansaru mnamo mwezi Januari lilitangaza kutengana na Boko Haram lakini maafisa wa usalama wanaamini kuwa bado ni kitu kimoja. Ansaru limeshukiwa kutekeleza  visa vya hivi karibuni katika eneo la kaskazini mwa Nigeria na Uingereza tayari imeliorodhesa kama kundi la kigaidi.

Maafisa wa usalama wa Nigeria bado wanaitafuta familia moja ya watu saba kutoka Ufaransa iliyotekwa nyara kaskazini mwa Cameroon na kuingizwa Nigeria na waasi wa Boko Haram.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef