RABAT: Watu watano wauwawa kwenye miripuko ya mabomu
11 Aprili 2007Watu wasiopungua watano waliuwawa jana wakati watu wawili wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa kiislamu walipojiripua mjini Casablanca. Watu takriban kumi walijeruhiwa kwenye miripuko hiyo.
Watuhumiwa watatu wa ugaidi walijiripua wakati polisi walipoivamia nyumba yao mjini humo.
Polisi wamesema mshukiwa mwengine aliyetambuliwa kama Mohamed Mentala, alipigwa risasi wakati alipokuwa akijiandaa kujiripua. Mentala ambaye amekuwa akitafutwa kuhusiana na mshambulio ya kujitoa mhanga masiaha ya mwaka wa 2003 alikufa alipopelekwa hospitalini.
Duru zinasema afisa mmoja wa polisi aliuwawa na mtoto mdogo kujeruhiwa.
Machafuko ya jana yalianza wakati polisi walipoizingira nyumba moja katika kitongoji cha Hay Farah mjini Casablanca baada ya kupewa taarifa na raia.