1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ra'ad Al Hussein asema hawezi kumnyenyekea Trump

Sylvia Mwehozi
21 Desemba 2017

Mkuu wa kamisheni ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein ambaye ni mkosoaji wa rais Donald Trump, amesema hatopunguza makali ya ukosoaji wake ili aweze kuchaguliwa tena katika nafasi yake hiyo.

https://p.dw.com/p/2pklu
Äthiopien DW-Interview UN-Menschenrechtler Seid al-Hussein
Picha: DW

Zeid Ra'ad Al Hussein amewaambia wafanyakazi siku ya Jumatano (20.12.2017) katika ujumbe wa barua pepe kwamba hawezi kujadiliana juu ya uadilifu wa shirika hilo mara utakapofika muda wa kuwania tena nafasi hiyo. Mapema wiki hii, wakati akifanyiwa mahojiano na shirika la habari la AFP, mwanamfalme huyo wa Jordan alikataa wazo la "kufanya hila" na wanasiasa ili aweze kuchaguliwa kwa kipindi cha pili, mjini Geneva.

Tangazo la kutowania tena nafasi yake 

Katika ujumbe wa barua pepe kwa wafanyakazi ambayo AFP, imefanikiwa kuipata, mkuu huyo aliandika kwamba, "baada ya kufikiria nimeamua kutowania kipindi cha pili cha miaka minne" akiongeza kwamba "katika muktadha huu wa siasa za kidunia" kusalia "kunaweza kukulazimisha kupiga goti la unyenyekevu, na kuzuia kauli ya utetezi". Hussein hakumtaja Trump kwa jina, lakini amekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres juu ya kulegeza ukosoaji wake wa haki za binadamu kwa Marekani.

Schweiz Genf Antonio Guterres
Antonio Gutterres na Zeid Ra'ad al HusseinPicha: picture-alliance/AP Photo/S. Di Nolfi

Hata wakati barua pepe yake imetambulika hadharani, Trump alikuwa akitishia kusitisha ufadhili wa Marekani kwa nchi zinazopingana na sera yake kuhusu Israel katika mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi. Wakati wa kampeni za Trump, Hussein alikosoa vikali ahadi ya mwanasiasa huyo mpya mwenye siasa kali za kizalendo, ya kupiga marufuku Waislamu kutembea au kuhamia nchini Marekani, akisema ni tabia isiyofaa.

Ukosoaji dhidi ya Trump

Mwezi Agosti, Hussein alimgeukia Trump,  juu ya repoti za vyombo vya habari alizoziita habari za uongo, akisema inaweza kuleta uchochezi dhidi ya waandishi wa habari. Alimlinganisha rais huyo wa Marekani na dereva wa gari anayelisongesha gari lake katika njia ya mlima. Katika mtazamo wa haki za binadamu, alisema anaonekana kuwa dereva asiyejali. Marekani inabaki kuwa mfadhili mkuu wa Umoja wa Mataifa na Gutterres amekuwa na nia ya kuendeleza mahusiano na utawala wa Marekani na pamoja na ajenda ya Umoja wa Mataifa.

Schweiz UN verurteilen brutale Massenvergewaltigungen im Südsudan
Zeid Ra'ad al Hussein na maafisa wengine wa Umoja wa MataifaPicha: Reuters/P. Albouy

Katika mahojiano na AFP, Hussein alipaza wasiwasi wake juu ya chama cha siaka kali za mrengo wa kulia katika serikali mpya ya mseto nchini Austria na kuwalenga wanasiasa ambao wako tayari kutumia hofu ili kujipatia madaraka ya kisiasa. Maoni ya Trump yanaonekana kupata sauti katika nchi nyingine ambako viongozi waliokuwa na mwelekeo wa kufunga mashirika ya kiraia au vyombo vya habari wanatumia lugha moja" alisema Hussein. Makundi ya haki za binadamu yamempongeza Hussein kwa msimamo wake mkali katika Umoja wa Mataifa ambaye alizungumza kwa uaminifu juu ya ukiukwaji wa haki nchini Syria, Myanmar miongoni mwa mizozo mingi.

Alikuwa afisa wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuielezea kampeni ya kijeshi nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya kama safisha safisha ya kikabila. Hussein mwenye miaka 53, mtaalamu wa diplomasia alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa mwaka 2014 na katibu mkuu wa zamani Ban Ki Moon, akichukua nafasi ya Navil Pillay wa Afrika Kusini. Alikuwa ni balozi wa Jordan katika Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2000 hadi 2007 na pia amehudumu kama afisa wa masuala ya kisiasa wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wa amani wa Umoja huo, wa iliyokuwa Yugoslavia wakati wa vita ya Balkan miaka ya 1990.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Saumu Yusuf