QUITO : Rais wa zamani kuondoka Ecuador leo
24 Aprili 2005Mzozo wa kidiplomasia kuhusu kiongozi wa zamani wa Ecuador Lucio Gutierrez unakaribia kabisa kupatiwa ufumbuzi leo hii kufuatia maelezo kutoka Brazil kwamba Rais huyo aliyen’golewa madarakani atasafirishwa kuondoka nchini humo kuelekea Brazil baadae leo hii.
Afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Brazil ameliambia shirika la habari la AFP mjini Brasilia hapo jana kwamba iwapo kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa Guiterrez atawasili Brazil hapo kesho na kwamba nchi hiyo inachukuwa hatua zote kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
Ndege ya jeshi la anga ya Brazil ilikuwa ikitarajiwa kuondoka kutoka Porto Velho kuelekea katika mji mkuu wa Quito nchini Ecuador kumchukuwa Rais huyo wa zamani ambaye amepatiwa hifadhi ya kisiasa nchini Brazili kufautia kundolewa kwake madarakani hapo Jumaatano kutokana na machafuko makubwa ya umma dhidi yake.
Maafisa wa serikali wamesema ndege hiyo imeruhusiwa kutuwa nchini humo licha ya upinzani wa wananchi walioko nje ya ubalozi wa Brazil mjini Quito ambako Guiterrez amejichimbia wakitaka kiongozi huyo atupwe gerezani badala ya kuachiliwa kuondoka nchini humo.