QUITO : Hatimae Rais wa Ecuador aondoka kuelekea Brazil
24 Aprili 2005Rais wa Ecuador aliyeondolewa madarakani Lucio Gutierrez ameondoka nchini humo leo hii kulekea Brazil alikopatiwa hifadhi ya kisiasa ikiwa ni siku nne baada ya kulazimishwa kuachilia madaraka kutokana na maadamano ya wiki moja barabarani dhidi ya serikali yake.
Polisi waliokuwa na silaha nzito walimuomdowa kwa siri Gutierrez na kumpeleka kwenye kituo cha anga kusini mwa Quito kutoka ubalozi wa Brazil ambako afisa huyo mstaafu wa jeshi alikuwa amekimbilia kujihifadhi baada ya kulitelekeza kasri la Rais wiki iliopita.
Waziri wa mambo ya ndani Mauricio Gandara ameiambia televisheni ya ndani ya nchi kwamba Guiterrez alisafirishwa hadi Latacunga na kutoka uwanja wa ndege wa Latacunga ameondoka kuelekea Brazil.
Bunge lilimtimuwa Guiterrez kwenye wadhifa wa Urais hapo Jumaatano baada ya kiongozi huyo kuutelekeza wadhifa huo na nafasi yake imechukuliwa na Makamo wa Rais Alfredo Alicio.
Guiterrez amekimbia baada ya jeshi kuacha kumuunga mkono na umati wa watu wenye hasira kumzuwiya kuondoka nchini humo.