PYONGYANG: Korea ya Kaskazini imefanya jaribo lake la kwanza la nyuklia
9 Oktoba 2006Korea ya Kaskazini imetangaza imefanya jaribio lake la kwanza la nyukilia. Jaribio hilo lililofanywa chini ya ardhi katika eneo la Hawadari, limefanyika kwa ufanisi mkubwa na hakukuwa na miale yoyote ya nyuklia iliyotoka kutoka kituo hicho.
Jumuiya ya kimataifa imekasirishwa na hatua hiyo ya Korea ya Kaskazini.
Katika matamshi ya kwanza ya Marekani, naibu kiongozi wa taasisi ya usalama wa kitaifa na sera za kigeni kwa maendeleo ya Marekani, Joseph Cirincione, amesema sera za Marekani zimeshindwa kuizuia Korea ya Kaskazini isifanye jaribio hilo la nyuklia.
Aidha amesema Marekani inaweza kupitisha azimio litakaloruhusu vikwazo vitumiwe kuilazimisha Korea ya Kaskazini irudi kwenye mazungumzo, lakini itakapokubali, litakuwa jukumu la Marekani ikubali pia kuzungumza nayo.
´Lazima tuwe tayari kuipa Korea Kaskazini vivutio kama tulivyoipa Libya. Achaneni na mpango wako wa nyuklia na tutawatambua, tutawahakikishia usalama na kuwapa misaada ya kiuchumi. Ni kushindwa kwetu kukamilisha makubaliano hayo, ndiko kulikosababisha mzozo huu kufikia ulipofikia hivi sasa.´
China imelipinga vikali jaribio hilo la nyuklia na imeitaka Korea ya Kaskazini itimize ahadi yake ya kutoeneza silaha za kinyuklia.
Waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, amesema jaribio hilo haliwezi kukubalika. Msemaji wa rais wa Korea Kusini amesema nchi yake itachukua hatua kali kulishughulikia swala hilo barabara.
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limelaani pia jaribio la nyuklia la Korea Kaskazini na limeitaka irudi kwenye mazungumzo.
Marekani imesema baraza hilo litatakiwa kuchukua hatua za dharura iwapo itathibitishwa rasmi kwamba Korea Kaskazini imefanya jaribio la nyuklia.