Putin na Erdogan kujadili mzozo wa Syria
3 Desemba 2012Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton , wakati huo huo ametoa onyo kali kwa utawala wa rais Bashar al-Assad kuhusiana na uwezekano wa kutumia silaha za kimekali dhidi ya waasi.
Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema kuwa makombora ya Syria yameshambulia maeneo katika wilaya ya Hajar al-Aswad na Tadamun pamoja na kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Yarmuk kusini mwa mji mkuu Damascus.
Putin akutana na Erdogan
Rais wa Urusi Vladimir Putin , wakati huo huo , alitarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wakati wa ziara ya kihistoria mjini Istanbul kujadili tofauti zao kuhusu Syria.
Mazungumzo hayo yametuwama katika "hali ya mapatano katika mashariki ya kati, hali katika ukanda wa Gaza, mzozo nchini Syria , pamoja na ushirikiano," mshauri ya masuala ya mambo ya kigeni wa Putin , Yury Ushakov amesema.
Uturuki na Urusi zimeingia katika mgongano kuhusiana na vipi inawezekana kuutatua mzozo nchini Syria ambapo serikali ya nchi hiyo inaendesha ukandamizaji wa wapinzani kwa nguvu na kusababisha umwagikaji mkubwa wa damu, licha ya ukuaji wa biashara pamoja na mahusiano katika sekta ya nishati.
Mvutano huo ulifikia kilele mwezi Oktoba mwaka huu baada ya Uturuki kuikamata ndege ya Syria iliyokuwa ikitokea Moscow kwenda Damascus , kwa tuhuma za kwamba ndege hiyo ilikuwa imebeba shehena ya silaha, na kusababisha jibu la hasira kutoka Urusi.
Watu 12 wauwawa
Mashambulio ya anga katika mji wa mpakani wa Ras al-Ain yamesababisha watu 12 kuuwawa na wengine zaidi ya 30 leo. Miongoni mwa waliofariki ni pamoja na watoto wanne na waasi wanane, limesema shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria.
Hali hiyo imesababisha ndege za kivita za Uturuki kupelekwa haraka katika eneo la mpakani.
Duru za usalama zimesema kuwa ndege za kivita chapa F-16 za uturuki zilipelekwa haraka kutoka katika kituo chake katika mji wa kusini mashariki ya Diyarbakir baada ya mashambulio ya anga katika makao makuu ya jeshi la ukombozi wa Syria katika mji wa Ras al-Ain, ikiwa ni onyo kwa Syria kutokiuka sheria ya mkapa na kuingia nchini Uturuki.
Waasi waliukamata mji huo kiasi mwezi mmoja uliopita katika mapigano ambayo yalisababisha makundi makubwa ya wakimbizi kuingia nchini Uturuki, na imekuwa ni jaribio katika uvumilivu wa Uturuki kuweza kujilinda dhidi ya ghasia kusambaa hadi katika ardhi yake.
Mwandishi: Sekione Kitojo/ rtre/afpe
Mhariri: Yusuf Saumu