Putin asema Poroshenko ana ‘mtazamo sahihi’
7 Juni 2014Baada ya kukutana na rais mteule, Petro Poroshenko, siku ya Ijumaa (tarehe 6 Juni), Putin alikubaliana na hatua za kiongozi huyo mpya kukomesha ghadia kwenye mikoa miwili iliyojitenga na Ukraine mashariki mwa nchi hiyo.
“Nimeupokea msimamo wa Bwana Poroshenko kwamba umwagaji damu mashariki mwa Ukraine lazima ukomeshwe mara moja,” alisema Putin baada ya mkutano uliofanyika kandoni mwa maadhimisho ya miaka 70 ya ushindi wa Vita vya Pili vya Dunia mjini Normandy. “Siwezi kusema kwa hakika vipi hilo litatekelezwa kiuhalisia, lakini kwa ujumla ninaona kwamba ni mtazamo sahihi.”
Hata hivyo, Rais Putin alisema anamngojea Poroshenko, ambaye ataapishwa leo Jumamosi, kutoa undani wa namna ya kutafuta suluhisho na kukomesha kwa msako dhidi ya makundi ya wale wanaotaka kujitenga. “Ukraine lazima ioneshe dhamira njema,” Putin aliiambia televisheni ya Urusi. “Operesheni ya ukandamizaji lazima ikomeshwe.”
‘Fursa nzuri' ya maendeleo
Poroshenko, ambaye alishinda takribani asilimia 58 ya kura kwenye uchaguzi wa tarehe 25 Mei, alisema anaamini kwamba kuanzishwa kwa mazungumzo na Urusi kutakuwa na matokeo mazuri, ambapo mazungumzo zaidi ya serikali mjini Moscow hayaepukiki.
“Majadiliano yameanza na hilo ni jambo jema,” alisema kupitia televisheni ya Ukraine. “Mwakilishi wa Urusi atakwenda Ukraine na tutajadiliana naye hatua za awali kuelekea mpango wa (kutatua) hali... Tuna fursa nzuri ya kuutekeleza.”
Viongozi hao wawili walipeana mikono na kuzungumza kwa dakika 15, huku Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakiwapo wakati wa mazungumzo hayo.
Katika siku za karibuni, hali ya wasiwasi imeongezeka mashariki mwa Ukraine, ambapo serikali ilithibitisha siku ya Alhamisi (tarehe 5 Juni) kwamba ilishapoteza udhibiti wa vituo vitatu vya mpakani kwa waasi. Afisa mmoja wa polisi aliuawa na wawili kujeruhiwa siku ya Ijumaa wakati kombora liliporushwa katika mji wa Slovyansk.
Mazungumzo muhimu
Putin pia alikutana na Rais Barack Obama wa Marekani siku ya Ijumaa, kwa mazungumzo mafupi yaliyochukua kiasi cha dakika 10 mpaka 15 kabla ya chakula cha mchana cha viongozi wengine wa dunia.
Mazungumzo hayo ambayo serikali ya Marekani iliyaita kuwa hayakuwa rasmi, Putin alisema yalikuwa na mjadala muhimu. Kabla na baada ya mkutano huo, vyombo vya habari viliwaelezea viongozi hao kwamba walikuwa wakikaribiana kwa tahadhari sana.
“Putin na Obama walizungumzia haja ya kukomeshwa kwa ghasia na mapigano haraka iwezekanavyo,” alisema msemaji wa Putin, Dmitry Peskov.
Mkutano huo wa Obama na Putin umekuja baada ya mkutano wa viongozi wa Kundi la Mataifa Saba yenye nguvu za kiviwanda duniani (G7) mjini Brussels. Viongozi hao wameitenga Urusi ambayo ilikuwa sehemu ya kundi la mataifa nane (G8) baada ya Urusi kuichukua Crimea mwezi Machi.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Sekione Kitojo