Putin aonesha 'kulainika' juu ya Syria
4 Septemba 2013Katika mahojiano na shirika la habari la AP na televisheni ya Urusi, First Channel, iliyotolewa leo ikiwa ni siku moja kabla ya mkutano wa viongozi wa G20 mjini St. Petersburg, Rais Putin amesema anatarajia kuzungumza na Rais Barack Obama wa Marekani kandoni mwa mkutano wa kilele juu ya suala la Syria, akisisitiza kwamba kuna mambo mengi ya wawili hao kujadiliana.
Wakati Putin alipoulizwa ikiwa nchi yake itakubaliana na hatua ya kijeshi endapo itabainika kuwa serikali ya Syria imefanya mashambulizi ya silaha za kemikali, alijibu kwa tahadhari ya hali ya juu.
"Sipuuzii uwezekano huo, lakini ningelipenda kukufahamisha jambo moja mahsusi tu. Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ni Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa peke yake linaloweza kuagiza matumizi ya nguvu dhidi ya dola huru. Mbinu au njia nyengine yoyote, inayoweza kutumika kuhalalisha matumizi ya nguvu dhidi ya dola huru, haukubaliki na utatafsiriwa tu kwamba ni uchokozi."
Kwenye Baraza la Usalama anakokutaja Putin, Urusi ina kura ya turufu na mara kadhaa imeitumia kuulinda utawala wa Assad. Katika mahojiano hayo, aliweka wazi kwamba nchi yake haiko tayari kukubaliana na kauli za Marekani na Ulaya kwamba vikosi vya Assad vilihusika na mashambulizi ya kemikali ya tarehe 21 Agosti, ambayo serikali ya Marekani yanasema yaliwaua zaidi ya watu 1,400.
"Hatuna taarifa halisi za kemikali hizo - hata bado haijahamika kama zilikuwa ni silaha za kemikali au ni kemikali tu zenye madhara na ikiwa kweli zilitumiwa na jeshi rasmi la serikali." Aliongeza Putin.
Marekani, Ufaransa kwenda vitani peke yao?
Tayari Marekani na Ufaransa zimeshasema kwamba zinajitayarisha kufanya mashambulizi bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa kwani zinaamini Urusi italipigia kura ya veto azimio la aina hiyo.
Mafungamano kati ya Marekani na Urusi yameingia dosari kubwa kabisa tangu kumalizika kwa Vita Baridi kutokana na masuala kadhaa, likiwemo la mapigano nchini Syria, ambako Urusi imekuwa muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Assad.
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Kimagharibi, amesema kwamba hata kama Urusi haitosema hadharani, kuna kila dalili kwamba maafisa wa Urusi wanaamini kwamba Assad anahusika na mashambulizi ya silaha za kemikali, na hilo limepunguza uungaji mkono wa Urusi kwake.
Wachambuzi wa mambo wanasema licha ya kuonesha tahadhari ya hali ya juu, kauli hii ya Putin inalenga kuonesha utayarifu wake kuyajenga tena mahusiano kati ya nchi yake na Marekani, licha ya Obama kuamua kujitoa kwenye mkutano wa kilele baina ya viongozi hao.
Obama, ambaye kwa sasa yuko nchini Sweden, anatarajiwa kuwasili mjini St. Petersburg hapo kesho akiwa amepata uungwaji mkono kutoroka kwa watu muhimu kwenye bunge la nchi yake katika mipango yake ya kuivamia Syria.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP
Mhariri: Josephat Charo