Putin akutana na Poroshenko
17 Oktoba 2014Viongozi hao wawili walikutana mapema Ijumaa (17 Oktoba) kandoni mwa mkutano wa kilele kati ya Ulaya na Asia kabla ya kufanya majadiliano makubwa zaidi na viongozi wa Umoja wa Ulaya ambao wametiwa shaka sana na ambavyo mzozo baina yao unavyoweza kuzua mtafaruku kwenye kiwango cha kimataifa.
Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, ambaye ndiye aliyeitisha mazungumzo hayo ya leo, yaliyofanyika kwenye ukumbi ulio mbali na ule unakofanyika mkutano wa kilele, amesema mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron. Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy na Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso, pia walihudhuria.
Muda mchache kabla ya kuingia kwenye ukumbi wa mkutano, Rais Poroshenko alisema mazungumzo hayo yalihusiana na ajenda zote muhimu ambazo zimezua mzozo kati ya nchi yake na Urusi kwa siku za hivi karibuni. "Masuala muhimu yakiwemo yale ya amani, kutekelezwa kwa ukamilifu makubaliano ya Misk, usitishaji mapigano, kuondoa wanajeshi na kuheshimiwa kwa mamlaka ya Ukraine, na kando ya hayo ni kutatuliwa kwa masuala ya nishati."
Renzi aliyaelezea mazungumzo hayo kuwa ya kutia moyo na kwamba ana matumaini ya kuukwamua mkwamo uliopo.
"Tulitaka kufikia mahala pa kuona kuwa kuna mabadiliko kwenye namna tunavyouzungumzia mzozo nchini Ukraine. Nadhani tumepiga hatua moja mbele kutokana na mazingira yaliyopo kwa maslahi ya majadiliano yanayojenga. Hapana shaka kwamba kuna tafauti nyingi. Hilo ni jambo la kawaida," alisema Renzi.
Urusi yasema mazungumzo magumu
Lakini msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov, aliyaelezea mazungumzo hayo kuwa ni magumu sana. Akizungumza na waandishi wa habari, Peskov alisema: "Mazungumzo haya kwa hakika ni magumu. Kuna suintafahamu nyingi na kiwango kikubwa cha kutokukubaliana. Hata hivyo yanaendelea."
Mataifa ya Magharibi yaliiwekea vikwazo Urusi kwa kuichukuwa kwake Rasi ya Crimea mapema mwaka huu na kwa kile wanachosema ni kuunga mkono kwake waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine. Mzozo huu unatajwa na wachambuzi kwamba unakaribiana sana na siasa za Vita Baridi.
Ulaya inahofia kwamba uamuzi wa Urusi kuikatia gesi Ukraine kwa sababu ya kutokulipia, kunaweza kuathiri mgao wa gesi kote barani Ulaya kwenye majira ya baridi yanayokaribia na sasa unapigania kufikiwa kwa makubaliano.
Urusi ndiye msambazaji mkubwa wa gesi kwa Ulaya, ikiwa inatoa kiasi cha robo nzima ya gesi inayotumika, huku nusu yake ikiwa inapitia Ukraine.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf