Putin aionya Magharibi kuhusu kitisho cha vita vya nyuklia
29 Februari 2024Akizungumza mjini Moscow katika hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa, Putin amesema wanajeshi wake wanaendelea kusonga mbele nchini Ukraine na kuzionya nchi za Magharibi kuhusu madhara makubwa kwa nchi yoyote itakayothubutu kuwapeleka askari nchini Ukraine.
"Nasi pia tunazo silaha, - wanajua kuhusu hili, kama nilivyosema hivi punde, - pia tuna silaha ambayo inaweza kuyapiga maeneo yao. Na (wanapaswa kuelewa) kwamba wanachokifanya sasa kujaribu kuutisha ulimwengu wote – kinaweza kuzusha mzozo wa silaha za nyuklia. Kumaanisha maangamizo ya ulimwengu. Je, hawaelewi hili, au nini?"
Kauli zake zimeonekana kuwa jibu kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye mapema wiki hii alikataa kufuta uwezekano wa kuwapeleka wanajeshi nchini Ukraine -- mtizamo ambao ulizusha upinzani wa haraka kutoka kwa viongozi wengine wa Ulaya.
Putin pia alipongeza hali nzuri ya kiuchumi ya Urusi na kuelezea mageuzi kadhaa madogo madogo ya ndani kama sehemu ya ahadi zake kwa Warusi kabla ya uchaguzi wa rais wa mwezi ujao ambao anatarajiwa kupata ushindi rahisi.