1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin ahutubia umati wa Warusi baada ya ushindi mnono

Hawa Bihoga
19 Machi 2024

Rais Vladmir Putin amesifu kurejea Urusi, kwa maeneo yalionyakuliwa kutoka Ukraine, baada ya kushinda uchaguzi uliotajwa na mataifa ya magharibi kuwa usio na uhalali.

https://p.dw.com/p/4dslg
Moscow, Urusi | Picha ya rais wa urusi ikipamba tamasha la  Red Square
Picha ya rais wa urusi ikipamba tamasha la Red Square mjini MoscowPicha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Jasusi huyo wa zamani alishinda asilimia 87 ya kura katika uchaguzi uliofanyika kwa siku tatu, ambao ulihusisha upigaji kura katika maeneo ya Ukraine yanayodhibitiwa na vikosi vya Urusi. 

Putin ambaye amekuwa madarakani tangu siku ya mwisho ya mwaka 1999, hivi anaelekea kuwa kiongozi alieitawala Urusi kwa muda mrefu zaidi katika kipindi cha zaidi ya karne mbili. 

Soma pia:Urusi yakosolewa kuandaa uchaguzi katika maeneo iliyoyanyakua Ukraine

Akizungumza katika tamasha la muziki lililoandaliwa kwenye Uwanja Mwekundu kuadhimisha miaka 10 tangu kutwaliwa kwa Rasi ya Crimea kutoka Ukraine, Putin alisema watasonga mbele pamoja na hii itawafanya kuwa imara zaidi. 

Alijigamba kwa kiunganishi kipya cha reli katika maeneo ya Ukraine yaliotekwa na vikosi vya Urusi, akisema maeneo hayo yalikuwa yametangaza shauku yake ya kurejea kwenye familia yao ya asili.