1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin afanya mazungumzo na Assad ya kutafuta amani Syria

Caro Robi
21 Novemba 2017

 Rais wa Urusi Vladimir Putin amekutana na Rais wa Syria Bashar al Assad mjini Sochi kabla ya mazungumzo siku ya Jumatano na viongozi wa Uturuki na Iran yanayolenga kuutia msukumo mchakato wa amani Syria.

https://p.dw.com/p/2nyYD
Russland Sotschi Treffen Assad und Putin
Picha: Reuters/Sputnik/M. Klimentyev

Ikulu ya Rais wa Urusi ya Kremlin imesema mkutano huo kwenye mji wa kitalii wa Sochi, umefanyika wakati wa kile kilichotajwa ziara ya kikazi ya Assad nchini Urusi. Putin amemsifu Assad kwa kupambana na ugaidi ambao amebashiri utaangamizwa nchini Syria.

Rais huyo wa Urusi amesema atashauriana na viongozi wengine wa dunia akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump na wa nchi za mashariki ya Kati kuhusu waliyoyajadili na Assad. Putin anatarajiwa kuzungumza na Trump Jumanne kupitia mawasiliano ya simu.

Vita vya Syria vyaelekea ukingoni?

Hapo kesho Jumatano, marais wa Urusi, Uturuki na Iran watakutana kwa mkutano wa kwanza kati ya msururu wa mikutano ya kilele inayonuia kuleta amani Syria, ambako wanajeshi wa serikali wamewazidi nguvu wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu-IS.

Russland Sotschi Treffen Assad und Putin
Rais wa Syria Bashar al Assad na wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/Sputnik/M. Klimentyev

Mazungumzo ya Putin na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na wa Iran Hassan Rouhani yatafanyika kabla ya kuanza mazungumzo yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa jijini Geneva tarehe  28 mwezi huu.

Hayo yanakuja huku Uturuki, Urusi na Iran zikishirikiana kuongeza juhudi za kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka sita na kusabababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu na kuwaacha mamilioni ya wengine bila ya makazi.

Ushirikiano huo unakuja licha ya kuwa Uturuki bado kimsingi ikiwa upande wa upinzani katika mzozo wa Syria. Urusi na Iran zimekuwa zikimuunga mkono Rais Assad tangu mwanzo wa mzozo huo.

Mnamo mwaka 2015, Urusi ilianzisha operesheni ya kijeshi Syria kumsaidia Assad na kubadili mkondo wa vita hivyo. Nchi nyingine ambazo zimekuwa zikiunga mkono upinzani Syria ni Marekani na nchi za ghuba.

Uturuki yashirikiana na Urusi na Iran

Nchi hizo tatu zimekuwa zikiunga mkono mazungumzo ambayo yamekuwa yakiendelea mjini Astana, nchini Kazakhistan ambayo yamewaleta katika meza ya mazungumzo mara saba mwaka huu, wawakilishi wa upinzani wanaotaka Assad kung'atuka madarakani na wa serikali.

Russland Moskau - Präsident Putin und Erdogan bei Pressekonferenz
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan na wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/S. Ilnitsky

Msururu huo wa mazungumzo umepelekea kutengwa maeneo salama nchini Syria ambako ghasia zimeripotiwa kupungua licha ya kuendelea kuwepo mapigano na miripuko ya mabomu ya hapa na pale. Urusi inalenga kuongoza mchakato wa kuutafutia ufumbuzi wa kisiasa mzozo wa Syria badala ya kutumia zaidi nguvu za kijeshi.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema mkutano wa kilele wa Sochi utasaidia kuanzisha tena mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya Syria na makundi kadhaa ya upinzani, wakati ambapo ushindi dhidi ya wanamgambo wa IS, unanukia.

Makundi kadhaa ya upinzani ya Syria yanakutana hapo kesho mjini Riyadh. Lengo la mazungumzo hayo yanayoongozwa na Saudi Arabia likiwa ni kufikia muafaka wa ajenda za mazungumzo ya wiki ijayo mjini Geneva, ambayo yatatuwama kuhusu katiba mpya na chaguzi Syria.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu