1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin asema mauaji ya balozi wake ni uchokozi

Sylvia Mwehozi
20 Desemba 2016

Afisa polisi wa Uturuki aliyekuwa akisema maneno ya "Allahu Akbar" na "Aleppo" amemshambulia kwa risasi na kumuua balozi wa Urusi nchini humo na kusababisha Rais Vladmir Putin kula kiapo cha hatua zaidi dhidi ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/2Ua9q
Türkei Anschlag auf russischen Botschafter
Picha: picture alliance/dpa/O. Ozbilici

Balozi Andrei Karlov alifariki dunia kutokana na majeraha ya kupigwa risasi mjini Ankara katika kituo cha maonesho ya sanaa. Shambulio lake limekuja wakati mawaziri wa kigeni wa mataifa hayo mawili pamoja na Iran wakikutana kwa mazungumzo muhimu mjini Moscow kuhusu mgogoro wa Syria.

Picha za tukio hilo zilimwonyesha mwanaume huyo akimmiminia risasi balozi huyo mgongoni wakati akifungua maonesho ya picha za Urusi. Mshambuliaji huyo aliyekuwa amevalia suti nyeusi, shati jeupe na tai alikuwa amesimama nyuma ya balozi na alijihami kwa silaha. Baada ya kumfyatulia risasi alisikika akitamka maneno ya "Allahu Akbar" yaani Mungu ni mkubwa na kisha akasema "usisahau kuhusu Syria, usisahau kuhusu Aleppo, wale wote walioshiriki katika dhuluma hii watawajibishwa".

Wizara ya mambo ya ndani ya Uturuki imemtambua mshambuliaji huyo kama Mevlut Mert Altintas, kijana mwenye miaka 22 aliyewahi kufanya kazi katika idara ya polisi ya kupambana na maandamano kwa kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita.

Archiv Putin und Karlov
Rais Vladmir Putin akiwa na balozi Andrei Karlov aliyeuawaPicha: Reuters/O. Orsal

Mauaji hayo yamekuja siku kadhaa baada ya kutokea kwa maandamano nchini Uturuki ya kupinga ushiriki wa Urusi nchini Syria, ingawa Moscow na Ankara kwa hivi sasa zinafanya kazi kwa pamoja katika kuwahamisha raia kutoka mjini Aleppo.

Rais Vladmir Putin wa Urusi ameyaita mauaji hayo kuwa ni "uchokozi" na kuongeza kuwa uhalifu huo pasi na shaka ni uchokozi unaolenga kuhujumu mahusiano baina ya Urusi na Uturuki pamoja na hatua za amani Syria zinazopiganiwa na Urusi, Uturuki, Iran na mataifa mengine yanayotaka kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa ndani wa Syria.

Putin amesema jawabu kubwa ni kuzidisha mapambano dhidi ya ugaidi wakati akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa matatu mjini Moscow.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameunga mkono kauli ya Putin akiahidi kuchukua hatua za pamoja katika uchunguzi wa mauaji hayo. "Uhusiano wetu na Urusi ni muhimu sana kwetu. Ni muhimu sana kwa ukanda wetu. Natoa wito kwa wote wanaotaka kuyadhoofisha mahusiano haya. Matarajio yenu yote hayatatimia, yatapotea. Tumethibitisha malengo yetu na tutaendelea na dhamira hiyo hiyo." amesema rais Erdogan.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na rais mteule wa Marekani Donald Trump ni miongoni mwa viongozi waliolaani mauaji hayo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi /AFP

Mhariri: Josephat Charo