Puigdemont aonya mzozo wa Catalonia huenda ukawa mbaya zaidi
26 Oktoba 2017Leo ni siku muhimu katika mzozo kati ya jimbo linalojitaka kujitenga na kujitawala la Catalonia na serikali kuu ya Uhispania. Bunge la jimbo la Catalonia linafanya kikao kuamua mustakabali wa jimbo hilo.
Kiongozi wa Catalonia Carles Puigdemont ameonya kuwa mzozo wa kisiasa unaojiri huenda ukawa mbaya zaidi iwapo serikali kuu ya Uhispania italipokonya jimbo hilo mamlaka ya kujitawala na kuongeza ni shambulizi dhidi ya katiba ya nchi.
Katika barua kwa baraza la seneti linalotarajiwa kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wa Catalonia hapo kesho, Puigdemont amesema serikali ambayo imeweka mazingira mabaya tayari, itajenga mazingira mabaya hata zaidi kwa kutwaa mamlaka ya kujitawala kwa Catalonia.
Puigdemont huenda akapunguza mzozo mkubwa wa kisiasa kuwahi kushuhudiwa Uhispania kwa miongo mingi kwa kuitisha chaguzi za mapema katika jimbo hilo au anaweza kupuuza onyo kutoka kwa serikali kuu na kutangaza rasmi uhuru wa kujitenga na kujitawala kwa Catalonia, jambo ambalo huenda likamfanya kufungwa gerezani.
Kikao cha bunge Barcelona
Uamuzi wake unatarajiwa kutangazwa katika kikao cha bunge kinachoanza leo Barcelona na huenda kikaendelea hadi kesho.
Vyovyote vile atakavyoamua, baraza la mawaziri la Catalonia linatarajiwa kuwa la kwanza la majimbo nchini Uhispania kuvunjiliwa mbali katika kipindi cha miongo minne iliyopita.
Hapo kesho, baraza la Seneti la Uhispania litakutana mjini Madrid ambako linatarajiwa kuidhinisha pendekezo la serikali kuu inayoongozwa na Waziri mkuu Mariano Rajoy kutaka kuitawala moja kwa moja Catalonia, jimbo lenye utajiri lililo na wakazi milioni 7.5 na pia kuidhinisha vikwazo vingine dhidi ya utawala wa Catalonia.
Mzozo huo kati ya Puigdemont na Rajoy kwa mara nyingine unatarajiwa kutokota leo. Puigdemont ambaye alihutubia bunge la jimbo hilo tarehe 10 mwezi huu, alisita kutangaza moja kwa moja uhuru wa kujitawala kwa Catalonia na badala yake alitaka kuwepo mazungumzo kati yake na serikali ya Rajoy. Hata hivyo vita vikali vya maneno vimeshuhudiwa kati ya pande hizo mbili.
Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Gakuba, Daniel