Puigdemont aishambulia vikali Uhispania
6 Novemba 2017Kiongozi aliyeondolewa madarakani wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont amelikemea taifa la Uhispania na kulitaja kama lilisilokuwa na demokrasia na ambayo pasi na haki imewakamata na kuwafunga jela wenzake. Matamshi ya Puigdemont ya kwanza tangu alipowachiliwa kwa dhamana nchini Belgium.
Puigdemont na wenzake 4 waliokuwa mawaziri waliachiliwa kwa masharti jumapili usiku baada ya kujisalimisha kwa mamlaka ya ubelgiji ili kukabiliana na kibali cha Hispania cha kukamatwa kwa mashtaka ya uasi na uchochezi.
"Tumetolewa bila ya dhamana .. mawazo yetu yako pamoja na wenzetu waliofungwa kidhulma na taifa ambalo liko mbali na kanuni za kidemokrasia," Puigdemont alisema kwenye mtandao wa twitter masaa machache baada ya wanasiasa hao watano kutolewa.
Alhamisi iliopita, jaji wa Uhispania mjini Madrid, aliamuru naibu wa Puigdemont' na mawaziri wengine saba wa Jimbo la Catalonia wazuiliwe kwasababu ya uwezekano wa kukimbia.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ubelgiji Didier Reynders alisisitiza kuwa ni jambo la kisheria na sio kwa wanasiasa kulishughulikia, licha ya Uhispania kukosolewa na wanachama wa jamii ya Flemish kutoka serikali yake mwenyewe.
"Tunapaswa kuruhusu mahakama ya Ubelgiji na Uhispania zifanye kazi zao," Reynders aliviambia vyombo vya habari vya Ubeligiji.
Puigdemont na washirika wake walikimbilia kwenda Ubelgiji wiki iliyopita baada ya Uhispania kumfukuza kiongozi huyo wa Catalan na kuweka utawala jimbo hilo katika mikono ya serikali kuu mjini Madrid, baada ya bunge lake kujitangazia uhuru mwezi uliopita.
Uhispania ilitoa vibali ulaya vya kukamatwa siku ya Ijumaa pale Puigdemont na washirika wake kupuuza ombi la kufika mbele ya hakimu kutokana na mashtaka yaliyohusishwa na hoja ya kutangaza Catalonia kuwa jimbo huru.
Chama cha PDeCAT cha Puigdemont kilisema Jumapili kuwa Puigdemont amejitokeza ili "kuonyesha nia ya kutokimbia mchakato wa mahakama na kujitetea katika mchakato utakao kuwa wa haki na usio na upendeleo huko Ubelgiji, na ni wa kutiliwa shaka nchini Uhispania.
Kesi nyengine itasikilizwa katika siku 15 sijazo. Ubelgiji ina hadi siku 60 kuamua kama itawarudisha wakatalani hao nyumbani.
Puigdemont, ambaye bado anajitaja mwenyewe kama "rais" wa Catalonia, amesema pia yuko tayari kuwania kama mgombea katika uchaguzi wa jimbo hilo Desemba 21 ulioitishwa na Waziri Mkuu Mariano Rajoy ili "kurejesha hali ya kawaida" katika jimbo la Catalonia.
Puigdemont amesema yeye na wenzake - Meritxell Serret, Antoni Comin, Lluis Puig na Clara Ponsati - watashirikiana na mamlaka ya Ubelgiji.
Puigdemont alikiri wiki iliyopita kwamba alikuwa amekwenda Ubelgiji kwa jitihada za kulipeleka suala la Catalonia katika Umoja wa Ulaya, ambayo imeiunga mkono Uhispania kwenye mgogoro huu.
Puigdemont, mwenye umri wa miaka 54, anasisitiza kuwa Catalonia ilipata haki ya kutangaza uhuru baada ya kura ya maoni na amewataja wenzake wanaozuiliwa kama "wafungwa wa kisiasa".
Jumapili iliopita , waandamanaji katika miji ya Catalonia waliandamana barabarani wakitaka waachiliwe.
Puigdemont alisema hajaridhika na hakikisho la kuwa na kesi yenye haki nyumbani Uhispania , akilaumu juu ya "shinikizo kubwa na ushawishi wa kisiasa kwa idara ya mahakama nchini humo ."
Jaji nchini Ubelgiji anaweza "kukataa kuamuru Puigdemont arudishwe nyumbani ikiwa kuna ushahidi kuwa haki za msingi zimo hatarini ," alisema Anne Weyembergh, rais wa Taasisi ya Utafiti wa Ulaya katika Chuo Kikuu Huria mjini Brussels.
Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman