PRETORIA: Haki za binadamu zapaswa kuheshimiwa
26 Juni 2005
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya,Jose
Manuel Barroso ameeleza masikitiko yake kuhusu msimamo wa Umoja wa Afrika wa kubakia kimya kuhusu Zimbabwe.Amesema,haki za binadamu lazima ziheshimiwe kama ni maadili ya kimataifa.Barroso alilijadili suala la Zimbabwe pamoja na Rais Thabo Mbeki wa Afrika ya Kusini,baada ya wakuu wa Umoja wa Afrika kusema kuwa hawana mpango wa kuijadili hali ya Zimbabwe kwa sababu hilo ni suala la ndani.Serikali ya rais Robert Mugabe wa Zimbabwe tangu majuma sita ya nyuma,imekuwa ikibomoa nyumba za masikini na wafanya biashara wasio na vibali.Kwa mujibu wa makundi yanayotetea haki za binadamu,hadi watu 300,000 hawana mahala pa kuishi wakati huu ambapo majira ya baridi yameanza katika nchi hiyo.Serikali ya Mugabe inasema,lengo la kampeni hiyo ni kukomesha biashara ya magendo na vitendo vingine visivyo halali.