Power kuzuru mataifa yaliyoathirika na Ebola
26 Oktoba 2014Wakati balozi huyo samantha Power akifanya ziara hiyo nchini mwake Marekani kuna miito inayoongezeka ya kutaka kuzuwia watu kutosafiri kwenda katika mataifa hayo kutoka Marekani.
Samantha Power atazizuru Liberia, Sierra Leone na Guinea , "kutoa msukumo kuhusu mahitaji ya kuiongeza misaada kutoka jumuiya ya kimataifa," imesema taarifa iliyotolewa jioni jana Jumamosi na ubalozi wa Marekani.
Msemaji wa balozi huyo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema Power amekwisha ondoka na anatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Guinea, Conakry , leo Jumapili (26.10.2014). Mapema jana Jumamosi , balozi huyo ametuma picha yake binafsi katika ukurasa wake wa Tweeter akiwa na balozi wa Guinea katika Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Mataifa umekuwa kila mara ukitoa miito ya kutolewa msaada zaidi na jumuiya ya kimataifa kupambana na ugonjwa huo hatari , ambao umesababisha vifo vya zaidi ya watu 4,900.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na Ebola ni wa kwanza kutayarishwa na taasisi hiyo ya kimataifa kama juhudi za kupambana katika mzozo wa kiafya wa jamii.
Power aisifu Cuba
Power amekuwa akizungumzia sana kuhusu haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti na jumuiya ya kimataifa dhidi ya ugonjwa huo hatari wa Ebola. Katika hotuba wiki iliyopita , ameisifu Cuba , nchi ambayo imekuwa chini ya vikwazo vya Marekani kwa miongo kadhaa, kwa kutuma madaktari 165 kwenda Sierra leone.
"Jumuiya ya kimataifa inashindwa nguvu na Ebola. Tunashindwa kuhimili mbio za Ebola," amesema katika hotuba.
Umoja wa Mataifa umeeleza wasi wasi wake wakati mashirika ya ndege na makampuni ya meli yamezuwia kutoa huduma zao katika mataifa hayo matatu ambayo yameathirika mno, na kufanya kuwa vigumu kupeleka wafanyakazi wa kutoa misaada pamoja na mahitaji na kusababisha bei za vyakula kupanda mno.
Wafanyakazi wenye ujuzi
Wafanyakazi wa kutoa misaada wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mengine pia wana wasiwasi juu ya changamoto za kuwavutia wafanyakazi wa kujitolea wenye ujuzi kuja kusaidia.
Taarifa ya Marekani imesema Power atazuru vituo vya taifa vya uratibu wa Ebola na kukutana na wafanyakazi wa Marekani na Umoja wa Mataifa katika nchi hizo zilizoathirika na ugonjwa Ebola.
Hii itajumuisha wafanyakazi wa vituo vya udhibiti na kuzuwia magonjwa na wizara ya ulinzi. Pia atakutana na maafisa wa serikali na wafanyakazi wa asasi za kijamii.
Taarifa hiyo hata hivyo haikusema iwapo Power atakutana na watu walionusurika na Ebola. Power pia atazuru Ghana, makao makuu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na Ebola na pia atakwenda Ubelgiji.
Safari ya balozi Power imetangazwa muda mfupi baada ya sera mpya za karantini kuanza kazi mjini New York wakati maafisa wakichukua hatua baada ya daktari kugundulika kuwa ameambukizwa virusi vya Ebola baada ya kuwatibu wagonjwa nchini Guinea.
Magavana wa New York, New Jersey na Illinois siku ya Ijumaa walitangaza karantini ya lazima ya siku 21 kwa wasafiri wanaowasili ambao wamehusika na wagonjwa wa Ebola katika mataifa ya Afrika magharibi.
Marekani imeahidi kutuma wanajeshi 4,000 kutayarisha vituo vya matibabu na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya katika eneo hilo lililoathirika mno.
Rais wa Marekani Barack Obama siku ya Jumatano amesema Marekani hadi sasa imekuwa na wafanyakazi 100 kutoka kituo cha udhibiti wa maradhi CDC na wanajeshi 500 wako katika mataifa ya Afrika magharibi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Caro Robi