Pompeo ziarani Mashariki ya Kati
24 Agosti 2020Pompeo alikutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ofisini kwake mjini Jerusalem, ambako walijadiliana makubaliano ya kihistoria ya hivi karibuni kati ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu chini ya usimamizi wa Marekani, ambayo yalitangaza kuanzishwa mahusiano ya kibalozi baina yao. Viongozi hao walitazamiwa pia kujadiliana juu ya Iran na China.
Mapema mwezi huu, Marekani, Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu zilitangaza makubaliano ya kuanzisha mahusiano kamili ya kibalozi, ambayo yanaitaka pia Israel kusitisha mipango yake ya kuzitwaa baadhi ya sehemu inazozikalia kimabavu kwenye Ukingo wa Magharibi, ambazo Wapalestina wanataka iwe ziwe sehemu ya taifa lao hapo baadaye.
Utawala wa Trump unayachukulia makubaliano hayo yanayokosolewa vikali na Palestina na washirika wake ulimwenguni kote kuwa mafanikio muhimu kwenye siasa zake za nje, katika wakati huu anapowania kutetea kiti chake kwenye uchaguzi wa Novemba.
Kwenye ziara yake ya leo, Pompeo alitazamiwa pia kukutana na mshirika wa Netanyahu kwenye serikali ya mseto, Waziri wa Ulinzi Benny Gantz, na pia Waziri wa Mambo ya Nje, Gabi Ashkenazi.
Safari ya Arabuni kote
Pompeo alipangiwa kuzizuru pia Sudan, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema huenda pia angelienda kwenye mataifa mengine ya Ghuba ikiwa italazimika.
Nchini Sudan, Pompeo alitazamiwa kushinikiza kuimarishwa kwa mahusiano kati ya nchi hiyo na Israel.
Msimamo wa kuichukia Iran walionao Marekani na Israel, kwa upande mmoja, na baadhi ya mataifa ya Kiarabu, kwa upande mwengine, unatajwa kuwa miongoni mwa sababu za mataifa hayo ya Kiarabu kukhalifu uungaji mkono wao wa asili kwa Wapalestina.
Muda mchache kabla ya kuwasili kwa Pompeo nchini Israel, jeshi la nchi hiyo lilifanya mashambulizi katika Ukanda wa Gaza, likidai kujibu mashambulizi ya maputo yaliyorushwa kutoka eneo hilo kuelekea Israel hapo jana.
Jeshi hilo lilisema kwamba lilivipiga mabomu vituo vya kijeshi na miundombinu ya chini ya ardhi inayomilikiwa na kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza.
Wanamgambo wenye mahusiano na kundi hilo wamefanya mashambulizi kadhaa ya maputo kwenye upande wa kusini mwa Israel katika siku za hivi karibuni, na kusababisha moto kwenye mashamba, wakilenga kuishinikiza Israel kuondowa mzingiro iliouweka dhidi ya Ukanda huo tangu mwaka 2007.