Pompeo kuelezea mipango ya Trump kuhusu Iran
29 Aprili 2018Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo aliwasili mjini Riyadh jana Jumamosi muda mfupi baada ya waasi wanaoungwa mkono na Iran wa Kihuthi nchini Yemen kufyatua kombora katika mpaka na nchi hiyo ya Kifalme.
Pompeo alikula chakula cha usiku pamoja na mrithi wa kiti cha Ufalme nchini Saudi Arabia Mohammed Bin Salman , na leo Jumapili alitarajiwa kukutana na baba yake mfalme Salman.
Baadaye alitarajiwa kusafiri kwenda Jerusalem kukutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na kisha atakwenda Amman Jordan, akikamilisha mazungumzo ya mwishoni mwa juma na baadhi ya mahasimu wakubwa wa Iran katika kanda hiyo.
Trump kusitisha makubaliano na Iran
Trump anatarajiwa hapo Mei 12 ama kurejesha vikwazo vya kinyuklia dhidi ya Tehran, na kuuweka mkataba huo wa mwaka 2015 katika mashaka, ambapo mataifa mengi yenye nguvu duniani yanauona kuwa muhimu katika kuizuwia Tehran kupata silaha za kinyuklia.
Lakini trump na washirika wa nchi hiyo katika mashariki ya kati wanadai makubaliano hayo yaliyoidhinishwa na mtangulizi wa Trump , Barack Obama , ni dhaifu mno na yanahitaji kubadilishwa na makubaliano mengine zaidi ya kudumu na kusaidiwa na udhibiti katika mpango wa Iran wa makombora.
Pompeo alianza ziara yake ya kwanza ya kidiplomasia ndani ya masaa mawili baada ya kuapishwa siku ya Alhamis na siku ya Ijumaa , baada ya mazungumzo na washirika wa NATO mjini Brussels, alionekana kudokeza kwamba Trump anapanga kusitisha makubaliano hayo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhriri: Yusra Buwayhid