1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo aishambulia China kwa kuziwekea nchi maskini madeni

19 Februari 2020

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, ameishambulia China kwa kutoa mikopo na kuziwekea nchi maskini mzigo mkubwa wa madeni.

https://p.dw.com/p/3Y0XH
Mike Pompeo  in Äthiopien
Picha: Getty Images/A. Caballero-Reynolds

Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imeanzisha hatua za kupunguza ushawishi wa China barani Afrika kwa kutumia mpango wake mpya wa maendeleo ya Afrika wa uwekezaji na biashara pamoja na shirika jipya la ufadhili wa maendeleo linalojulikana kama shirika la kimataifa la ufadhili wa maendeleo la Marekani.

Wachambuzi wanasema, shirika hilo ni juhudi za Marekani za kutoa njia mbadala kwa mpango wa China wa barabara unaonuia kuiunganisha China kupitia bahari na ardhini na Kusini Mashariki na Kati mwa Asia, Mashariki ya Kati na Afrika.

Katika taarifa aliyotoa kwa viongozi wa kibiashara nchini Ethiopia, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amezitaja kampuni kama Chevron, Coca cola na Bechtel kama wawekezaji wakubwa katika bara la Afrika. Amethibitisha pia kuwa Marekani inatafuta mkataba wa biashara huria na Kenya lakini hakutoa habari mpya kuhusu mazungumzo yalioanza mapema mwezi huu nchini Marekani.

Mike Pompeo in Angola
Mike Pompeo akutana na waziri wa mambo ya nje wa Angola Manuel Domingos Augusto nchini AngolaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Caballero-Reynolds

Pompeo amesema kuwa serikali  ya Rais Trump inataka ushirikiano huu wa kibiashara kuendelea na kupanuka. Tumejitolea kutimiza hayo. Kama kuna kitu mnapaswa kuelewa kuhusu rais wetu- mwajiri wangu - unapaswa kuelewa kuwa anapenda mikataba. Anataka mengi kufanyika . Anataka mengi kufanyika kati ya Marekani na mataifa yote barani Afrika

Kwa mujibu wa Kjetil Tronvoll, mtaalamu wa masuala ya Ethiopia kutoka chuo kikuu cha Bjorknes  mjini Oslo, ziara ya Pompeo nchini Ethiopia pia ilipangwa kuonyesha uungaji mkono wa mageuzi ya kisiasa ya waziri mkuu Abiy Ahmed licha ya visa vya ghasia za kisiasa.

Ethiopia inatarajiwa kuandaa uchaguzi Agosti 29 na Abiy ameahidi kuandaa uchaguzi huru na haki tofauti na miongo iliyopita ya ukandamizaji. Ethiopia ilikuwa kituo cha tatu cha ziara ya waziri Pompeo katika mataifa ya Afrika, ambayo ilimfikisha pia katika mataifa ya Senegal na Angola. Wachambuzi wamesema mbali na ushirikiano wa kibiashara, ziara ya waziri huyo ililenga pia kupeleka ujumbe tofauti na hatua za Marekani za hivi karibuni kuhusu Afrika, ambazo miongoni mwa mambo mengine ni vikwazo vya viza kwa raia wa nchi ne za bara hilo ambazo ni  Nigeria, Sudan, Tanzania na Eritrea.