Polisi yauwa waandamanaji 4 Bahrain
17 Februari 2011Katika pambano hayo mbali ya kuuawa kwa waandamanaji hao, wengine kiasi ya 95 walikamatwa na polisi.
Waandamanaji hao wanaodai demokrasia, na wakihamasishwa na mafanikio ya nguvu ya umma huko Tunisia na Misri, waliandamana kuelekea katika uwanja wa Pearl mjini Manama.Katika eneo hilo kwa siku ya nne sasa wapinzani hao wamekuwa hapo katika kuchagiza madai yao.
Fadel Ahmed mmoja waandamanaji hao amesema kuwa bila ya taarifa yoyote au onyo lolote, askari walivamia eneo hilo na kuanza kuwashambulia kwa mabomu na virungu.
Katika hospitali kuu ya Salmaniya mjini humo, idadi ya majeruhi ilikuwa kubwa kuliko uwezo wa hospitali hiyo, huku magari ya wagonjwa na yale ya binafsi yakiendelea kupeleka watu waliyojeruhiwa.Ndugu na jamaa za majeruhi na waliyokufa walikusanyika nje ya hospitali hiyo huku wakilia kwa uchungu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Bahrain Jenerali Tarek al-Hassan katika taarifa yake alisema kuwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimefanikiwa kulisafisha na kuwafurusha waandamanaji kutoka katika eneo hilo la uwanja wa Pearl, hiyo ikiwa ni baada ya kushindwa kwa juhudi zote za kidiplomasia kuwataka waandamanaji kuondoka hapo.
Kwa upande wake kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha kishia cha Islamic National Accord Association (INAA) alilaani operesheni hiyo akisema ni shambulio dhidi ya watu waliyokusanyika kwa amani.Amesema hatua hiyo itakuwa na madhara makubwa kwa uimara wa Bahrain.
Marekani kupitia msemaji wa serikali ya nchi hiyo Jay Carney imetaka kuheshimiwa kwa haki za wananchi kuandamana kwa amani kutaka kusikilizwa kwa madai yao.
Maandamano ya kutaka mabadiliko ya kidemokrasia pia yamezikumba nchi za Jordan ambako hapo jana kiasi ya watu 1,500 waliandamana katika mji wa Irbid uliyoko kaskazini mwa nchi hiyo.
Nchini Yemen waandamanaji leo walitarajiwa kuingia mitaani katika mji mkuu Sanaa, baada ya hapo jana waandamanaji wengine kupambana na polisi katika mji wa Aden nchini humo.
Wimbi hilo la kutaka mabadiliko ya kidemokrasia linaonekana kusambaa katika ulimwengu wa mataifa ya kiarabu, ambapo, mchambuzi mmoja wa masuala ya kisiasa nchini Saudi Arabia Khaled Dakheel anaonya kuwa eneo hilo linakabiliwa na athari za kile kilichotokea Tunisia na Misri.
Kati ya nchi sita katika eneo la Ghuba zinazoongozwa kifalme, ni Kuwait pekee ina bunge lililochaguliwa ambalo lina nguvu.Bahrain ina bunge ambalo kazi ni kutathmini na kupitisha sheria zilizopendekezwa na mfalme au baraza la mawaziri.
Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/Reuters/ZPR
Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman