Polisi yatawanya waandamanaji, DRC
21 Januari 2018Mwandishi habari wa shirika la habari la Reuters alishuhudia polisi na majeshi ya ulinzi yakifyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi hewani nje ya kanisa kuu la mjini Kinshasa Notre Dame. Kiasi watu sita wamejeruhiwa kidogo wakati walipopigwa na makopo ya mabomu ya kutoa machozi yaliyokuwa yakiruka huku na kule. Maandamano hayo yaliandaliwa na kanisa Katoliki.
Hasira zimekuwa zikiongezeka dhidi ya Kabila tangu pale alipokataa kujiondoa madarakani mwishoni mwa muhula wake kisheria Desemba 2016, na kuzusha maandamano mitaani ambapo watu kadhaa waliuwawa mjini Kinshasa, na kusababisha kuwapo kwa makundi kadhaa ya waasi katika maeneo mengine ya nchi hiyo.
Hali hii imeongeza hofu kwamba , taifa hilo kubwa lenye utajiri mkubwa wa madini huenda likarejea tena katika vita ambavyo vimewauwa mamilioni ya watu katika miaka ya 1990, wengi wao kutokana na njaa na magonjwa.
"Nimeandamana leo kwa sababu tu: Nataka kuwalea watoto wangu katika nchi ambayo inaheshimu haki za binadamu," muandamanaji Pascal Kabeya , mwenye umri wa miaka 40 mchuuzi katika soko , aliliambia shirika la habari la Reuters mahali ambapo mamia kadhaa ya watu walijikusanya katika kitongoji cha mjini Kinshasa.
Kanisa Katoliki
Georges Kapiamba , rais wa chama kinachotoa usaidizi wa Kisheria nchini Congo, Congolese Association for Access to Justice (ACAJ)kimesema idadi ya watu waliouwawa kuwa ni watatu na wengine 17 wamejeruhiwa. Msemaji wa polisi hakuweza kupatikana mara moja kwa ajili ya kutoa maelezo.
Ghasia zimekuwa kama zile za mkesha wa mwaka mpya, wakati majeshi ya Congo yalipowauwa watu saba katika mji mkuu wakati wa maandamano ya wanaharakati wa Kikatoliki.
Katika makubaliano baina ya kanisa Katoliki na wapinzani wa Kabila, rais alitakiwa kujiuzulu mwishoni mwa mwaka jana, akisafisha njia kwa ajili ya uchaguzi uliotarajiwa kufanyika mapema mwaka huu. Lakini alikaidi makubaliano hayo na uchaguzi umekuwa ukicheleweshwa mara kwa mara , na sasa unatarajiwa bila uhakika kufanyika mwishoni mwa mwaka huu 2018.
Kanisa Katoliki limejitokeza tangu wakati huo kuwakumbatia wapinzani wa juhudi za Kabila kuendelea kubaki madarakani bila kuwa na uhalali huo, wakati upinzani wa kisiasa ukiwa bado dhaifu na umegawanyika.
Kabila , ambaye amekuwa rais baada ya baba yake kuuwawa mwaka 2001, anatupa lawama za ucheleweshaji huo wa uchaguzi kwa utaratibu wa uandikishaji wa wapiga kura.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Isaac Gamba