Polisi ya Ujerumani yaufunga msikiti wa Hamburg
9 Agosti 2010
Polisi ya Ujerumani leo imeufunga msikiti wa mjini Hamburg ambao mnamo miaka ya nyuma ulihusishwa na mashambulio ya kigaidi ya tarehe 11 mwezi septemba nchini Marekani.
Polisi imesema msikiti huo una mahusiano na makundi ya wapiganaji wenye itikadi kali za kiislamu ya nchini Pakistan na Afghanistan.
Polisi ya Ujerumani imeeleza kwamba kwa muda wa miaka mingi msikiti huo ulikuwa mahala ambapo waislamu wenye itikadi kali wamekuwa wanakutana.
Aliekuwa kiongozi wa mashambulio ya tarehe 11 mwezi Septemba nchini Marekani, kwa niaba ya alkaida, Mahammed Atta, alikuwa anasali kwenye msikiti huo mara kwa mara.
Kwa muda mrefu nyumba hiyo ya ibada imekuwa inamulikwa na idara za usalama za Ujerumani.
Seneta wa mambo ya ndani wa jimbo la Hamburg, Christoph Ahlhaus, amesema jimbo la Hamburg halitaruhusu kuwepo kituo cha mikutano ya kundi la watu wanaotaka kujengwa kwa mfumo wa itikadi kali ya kiislamu kwa kutumia njia za nguvu.Amesema vyama vinavyotumia njia za mabavu kupinga mfumo wa kikatiba na siasa ya kuleta uelewano baina ya mataifa haviwezi kuruhusiwa katika jiji la Hamburg.
Idara ya mambo ya ndani ya jimbo la Hamburg ilitoa amri ya kuufunga msikiti huo mapema leo asubuhi.Maafisa wa polisi walizipekua nyumba na makaazi ya viongozi wa jumuiya ya msikiti huo ambao hapo awali ulikuwa unaitwa msikiti wa Al Quds kabla ya kubadilishwa na kuitwa msikiti wa Taiba.
Mali za jumuiya ya msikiti huo zimetwaliwa na polisi.Jumuiya iliyokuwa inaudhamini msikiti huo pia imepigwa marufuku.
Mwandishi/ Corall AstridARD/ZDF
Tafsiri:Mtullya Abdu
Mhariri: Miraji Othman