Polisi ya Pakistan yapambana na wafuasi wa Khan
11 Februari 2024Duru zinasema polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji huko Rawalpindi, Kusini mwa mji mkuu Islamabad na katika mji wa mashariki wa Lahore. Maandamano yamefanyika pia kwenye maeneo mengine bila rapsha yoyote.
Soma pia:Wanasiasa walioungwa mkono na Khan washinda vita vya bunge Pakistan
Mwenyekiti wa chama hicho cha Tehreek-e-Insaf (PTI) Gohar Ali Khan, aliwaambia waandishi habari hapo jana kwamba vitendo vya udanganyifu kwenye uchaguzi vimefanyika kila kona ya nchi hiyo. Aliwatolea mwito wafuasi wa chama hicho kuingia mitaani leo kuonesha upinzani wao.
Pakistan inatishiwa na mkwamo wa kisiasa
Katika uchaguzi huo ambao matokeo yake ya mwisho yametangazwa leo, wagombea binafasi wenye mafungamano na Khan wameshinda viti vingi bungeni. Lakini hawawezi kuunda serikali, hali inayotishia kuitumbukiza Pakistan kwenye mkwamo wa kisiasa wakati vyama hasimu vimeanza mazungumzo ya kujaribu kuunganisha nguvu kupata serikali ya mseto.