Polisi watembea kwa miguu kwa ukosefu wa petroli Zimbabwe
13 Januari 2019Zimbabwe imeongeza zaidi ya mara mbili bei ya mafuta, hatua ambayo inahatarisha maisha kuwa magumu kwa wananchi wake walio wengi ambao tayari wanakabiliana na hali mbaya ya uchumi inayoshuhudiwa nchini humo. Rais Emmerson Mnangagwa ametangaza kupitia mtandao wa Facebook Jumapili (13.01.2019) kwamba kutokana na ukosefu wa mafuta uliopo hivi sasa katika soko la nchi hiyo wameamua kuchukua hatua stahiki. Mafuta ya Diesel yatapanda hadi kufikia dalla 3.11 kwa lita wakati Petroli ikiuzwa kwa dolla 3.33 kwa lita moja kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao rasmi wa rais huyo.
Awali Petroli ilikuwa ikiuzwa dolla 1.32 kwa lita kwa mujibu wa mwandishi habari wa shirika la kijerumani la dpa mjini Harare. Misururu mirefu imeonekana nje ya vituo vya mafuta katika mji mkuu Harare huku ikitajwa kwamba baadhi ya watu wamelala kwenye magari yao ili kulinda nafasi zao katika misururu hiyo ya kusubiri kununua mafuta. Hatua ya Mnangagwa inakusudia kuyamaliza matatizo makubwa yanayozidi kuchochea hasira za wananchi huku yeye mwenyewe akiwa ameshaondoka akielekea katika ziara yake Urusi na nchi nyingine kwa ajili ya kutafuta wawekezaji.
Katika mkutano na waandishi habari alioufanya Jumamosi usiku rais Mnangagwe alifafanua kwamba hatua ya kuongezwa bei ya mafuta inayodhibitiwa na serikali inapaswa kuyapunguza matatizo yanayoikumba nchi katika wiki za karibuni. Rais huyo ameondoka leo Jumapili kuelekea kwenye ziara yake ambayo pia itamfikisha kwenye mkutano wa kimataifa juu ya uchumi huko Davos Uswisi. Lakini wakosoaji wenye ghadhabu wanasema Mnangagwa alitakiwa kubakia nchi mwake ili kushughulikia mgogoro uliopo. Ukosefu wa mafuta ya petroli katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika unaonesha ni kwa jinsi gani inavyokabiliwa na mgogoro mbaya wa kiuchumi kwa kipindi cha muongo mmoja kufuatia ukosefu mkubwa wa safaru za kigeni.
Ukosefu huo wa mafuta unaaminisha kwamba polisi wanalazimika kutembea mwendo wa kilomita chungunzima kwa miguu wakiwa wamewakamata watuhumiwa kutokana na magari yao kukosa mafuta. Si tu magari ya polisi lakini hata magari ya kubeba wagonjwa,mabasi ya shule,magari ya usafiri wa umma na hata magari ya kubeba taka yamejikuta yakipanga foleni kwenye misururu mirefu ya kusubiria mafuta kwenye vituo vya mafuta.
Mgogoro huu wa ukosefu wa mafuta ni sehemu tu ya matatizo makubwa ya kiuchumi yanayoikabili Zimbabwe ambayo rais wao Mnangagwa aliwapa kwa muda matumaini baada ya kutwaa madaraka kutoka kwa rais Robert Mugabe kwa kusaidiwa na jeshi Novemba 2017. Ikumbukwe kwamba punde baada ya rais huyo kuingia madarakani Zimbabawe iliingia katika mfumuko mkubwa wa bei uliopanda hadi kufikia asilimia 31 kiwango ambacho ni kikubwa mno kuwahi kutokea tangu 2009 huku kukiweko upungufu wa sarafu za kigeni.
Zimbabwe ilalazimika kuachana na sarafu yake mwaka 2009 baada ya kuzuka mfumko mkubwa wa bei uliofikia asilimia bilioni 500 kwa mujibu wa shirika la fedha la kimataifa IMF. Tangu wakati huo dolla ya Marekani ndiyo iliyohodhi katika shughuli zote za biashara za nchi hiyo. Lakini sasa kutokana na upungufu wa sarafu hiyo ya kigeni watu wengi wanalazimika kutumia noti maalum zilizochapishwa na serikali ambazo zilitakiwa kuwa na thamani sawa na dola. Lakini katika soko la fedha la magendo fedha hizo zinashuka haraka thamani yake dhidi ya Dolla.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Lilian Mtono