Polisi watano wauawa kwa risasi Dallas
8 Julai 2016Wadunguaji wamewaua maafisa 5 wa polisi katika mji wa Dallas nchini Marekani na kuwajeruhi wengine 6 katika mashambulizi ambayo Rais Barack Obama ameyaita ya kikatili na yaliyopangwa. Mauaji yametokea wakati wa maandamano ya amani ya kulaani kuuawa kwa Wamarekani wawili wenye asili ya Afrika kulikofanywa na polisi kwenye mji huo huo, masaa machache kabla.
Washambuliaji hao wa kulenga shabaha, walianza kuwafyatulia polisi risasi saa tatu kasorobo majira ya Marekani, usiku wa kuamkia leo, wakati mamia ya waandamanaji wakikusanyika kupinga visa viwili vya hivi punde, vya polisi kudaiwa kuwapiga risasi watu weusi na kuwaua.
Akizungumzia mauaji hayo akiwa mjini Warsaw, Poland, anakohudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Rais Barack Obama wa Marekani amesema hakuna namna hata moja ya kuhalalisha mauaji kama hayo, na akaapa sheria kuchukuwa mkondo wake. "Tunajua watu wakijihami kwa silaha hatari, wanaweza kufanya maangamizi kama haya..."
Polisi inasema mmoja wa washukiwa waliokuwa wakijibizana kwa risasi katika makabiliano hayo ameuawa na pia imemuachia huru mshukiwa mwengine ambaye awali alishikiliwa baada ya kujipeleka mwenyewe mikononi mwa polisi. Kwa mujibu wa polisi, licha ya mshukiwa huyo Mark Hughes, kushiriki kwenye maandamano ya amani ya Dalls akiwa na silaha, lakini hakufyatua risasi yoyote.
Hofu ingali imetanda eneo hilo, huku polisi wakiendelea kuwa katika tahadhari kuu kufuatia madai ya mshambujiaji kuwa kuna mabomu eneo hilo. Hata hivyo polisi imefanya ukaguzi na kubaini kuwa hamna mabomu japo inaendelea na upekuzi zaidi.
Ghadhabu za kuuawa kwa watu weusi Marekani
Awali akizungumza kwenye eneo la tukio wakati polisi ikiendelea na operesheni ya kuwakamata washukiwa, mkuu wa polisi wa Dallas, David Brown, alisema walikuwa wanafanya kila wawezalo kulimaliza suala hili kwa njia salama zaidi: "Mshukiwa ambaye tunazungumza naye ambaye pia ametukabili kwa risasi kwa zaidi ya dakika 45 ameambia wazungumzaji wetu kuwa mwisho unakaribia na atadhuru na kuua wengi wetu, na kwamba kuna mabomu kila mahali eneo hilo, hivyo tunachukua tahadhari kuu katika mbinu zetu ili tusidhuru maafisa wetu pamoja na raia wa Dallas tukiendelea kumhusisha kwenye mazungumzo.
Maandamano ya amani yalifanywa katika miji kadhaa nchini Marekani usiku wa Alhamisi kulaani kisa cha polisi wa Minnesota kumpiga risasi mtu mweusi Philando Castile aliyekuwa ndani ya gari na kumuua, pamoja na mtu mwengine kwa jina Alton Sterling aliyepigwa risasi na kuuawa na polisi eneo la Louisiana.
Polisi imesema mshambulizi alieleza kuwa alifanya shambulio hilo kutokana na ghadhabu za polisi kuua watu weusi nchini humo na kulaumu mfumo wa sheria wa Marekani kwa kuwadharau.
Mwandishi: John Juma/APE/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef