1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wamtaja mshambuliaji wa tatu

6 Juni 2017

Polisi nchini Uingereza imemtambulisha mshambuliaji wa tatu baada ya shambulio la mjini London. Uchunguzi mpya bado unaendelea. Suala la usalama limepamba moto kwenye kampenni za uchaguzi

https://p.dw.com/p/2eD1F
London Gedenkfeier für Opfer des Attentats
Picha: Getty Images/AFP/D. Leal-Olivas

Polisi wa Uingereza wamemtambulisha mtu huyo kuwa ni Youssef Zaghba mwenye umri wa miaka 22 anayeaminiwa kuwa ni raia wa Italia mwenye asili ya Kimoroko. Polisi vilevile wameeleza kuwa Zaghba alikuwa anaishi Mashariki ya London na kwamba familia yake tayari imeshajulishwa. Lakini wakati huo huo polisi wamefahamisha kwamba mtu huyo sio mshukiwa mkuu katika uchunguzi wao.

Washambuliaji wengine wawili walitajwa hapo awali kuwa ni Khuran Shazad Butt raia wa Uingereza mzaliwa wa Pakistan aliyekuwa na umri wa miaka 27 na Rachid Redouane aliyekuwa na umri wa miaka 30 aliyekuwa na uraia pacha wa Libya na Morocco. Washambuliaji hao watatu walikuwa wamevaa fulana za vilipuzi ambazo baadaye ilifahamika zilikuwa za bandia baada ya kupigwa risasi na kuuwawa na polisi.  Watu hao waliendesha gari kwa mwendo wa kasi na kuwagonga wapita njia katika darala la mjini London na kisha waliwachoma watu kwa visu waliokuwa karibu na soko la Borough.  Wakati wa mashambulio hayo watu saba waliuwawa na wengine kadhaa walijeruhiwa.

London Trauer nach Anschlag vom 03.05.2017
Raia wakiweka mashada ya mauwaPicha: Imago/ZUMA Press/T. Akmen

Shambulio hilo likiwa ni latu kutokea nchini Uingereza limezua maswali juu ya uwezo wa serikali ya waziri mkuu Theresa May katika kuwalinda raia wake hasa ukizingatia kupunguzwa kwa idadi ya polisi nchini humo katika miaka ya hivi karibuni. Suala la usalama limekuwa ni mwiba katika kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika siku ya Alhamisi tarehe 8. Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May katika jaribio la kuwatuliza watu ameahidi kuwapa nguvu zaidi polisi na pia kupambana na maudhui yenye msimamo mkali katika mitandao ya Intaneti.  Gazeti moja la nchini Italia limeripoti kwamba mtuhumiwa huyo wa tatu mnamo mwaka 2016  alizuwiwa nchini Italia alipokuwa anajaribu kwenda nchini Syria. Wakati huo huo polisi mjini London wamesema watuhumiwa wote 12 waliokuwa wamekamatwa hapo awali wameachiwa. 

Kiwango cha hali ya usalama nchini Uingereza bado kipo kwenye hali ya hatari hii ina maana huenda shambulio jingine la kigadi likatokea.  Polisi vilevile wamesema shambulio la London halihusiani na shambulio la Manchester la tarehe 22 mwezi uliopita.

Mwandishi: Zainab AzizIAPE/AFPE

Mhariri:Iddi Ssessanga