1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wamtafuta mshukiwa wa shambulizi la Berlin

Josephat Charo
21 Desemba 2016

Polisi nchini Ujerumani wanafanya msako kumtafuta mtu mmoja au zaidi wanaoshukiwa kufanya shambulio mjini Berlin, baada ya kumuachia mshukiwa mmoja waliyekuwa wamemkamata.

https://p.dw.com/p/2UdvJ
Deutschland Sicherheit Weihnachtsmarkt Polizei
Picha: picture alliance/dpa/C. Charisius

Polisi wanapanga kufanya operesheni katika jimbo la North Rhein Westphalia magharibi ya Ujerumani kuhusiana na shambulizi la lori lililofanywa katika soko la Krismasi mjini Berlin. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa za shirika la habari la Ujerumani, dpa, zikizikuu duru za usalama. Taarifa hizo zimefichuliwa muda mfupi baada ya taarifa za vyombo vya habari kusema polisi walikuwa wakimtafuta mshukiwa raia wa Tunisia ambaye hati zake za uhamiaji zilipatikana ndani ya lori hilo.

Gazeti la Allgemeine Zeitung limeripoti kwamba mhamiaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anayetafuta kibali cha uhamiaji anafahamika kwa maafisa wa usalana kwa makosa mengine, lakini halikutoa maelezo zaidi wala kutaja vyanzo vya habari hizo.

Juhudi za uchunguzi zaongezwa

Polisi wa Ujerumani wameongeza juhudi za kumtafuta dereva wa lori aliyeliendesha kwa kasi kulielekeza ndani ya soko la Krismasi Jumatatu usiku, katika shambulizi lililodaiwa kufanywa na kundi linalojiita Dola la kiislamu IS. Waendesha mashitaka wa shirikisho waliamuachia huru mshukiwa pekee, raia wa Pakistan mwenye umri wa miaka 23 anayetafuta kibali cha uhamiaji, baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha kwamba alihusika katika shambulizi hilo.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, alisema kuna ishara nyingi zinazoonyesha mhamiaji huyo hakuhusika na hujuma hiyo na kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa mshambuliaji halisi alitoroka na hivyo uchunguzi unaendelea. Akizungumza na kituo cha televisheni cha ZDF waziri huyo pia alisema hatua madhubuti zitachukuliwa kuyalinda masoko ya Krismasi Ujerumani.

"Katika siku zijazo tutayalinda vyema zaidi masoko ya Krismasi. Haya ni makubaliano yaliyoafikiwa kati ya serikali kuu na mawaziri wa mambo ya ndani wa serikali za majimbo. Tulitafakari kuyafunga masoko ya Krismasi lakini tukaamua tusifanye hivyo. Masoko haya yana umuhimu mkubwa kwetu na ni utamaduni wetu wa Kikristo. Hatutaki kushindwa na ugaidi. Tunafahamu hakuna ulinzi kamili, hata wataalamu wakijaribu kutushauri."

Deutschland PK Thomas De Maziere über Anschlag in Berlin
Waziri wa mambo ya ndani, Thomas de MaizierePicha: Getty Images/AFP/J. McDougall

Mshukiwa kupatikana haraka

Shambulizi dhidi ya soko la Krismasi karibu na kanisa la makumbusho la Kaiser Wilhelm katikati mwa mji mkuu Berlin lilisababisha vifo vya watu 12 na wengine karibu 50 kujeruhiwa. Majeruhi 24 wametibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Mkuu wa jeshi la polisi wa Berlin, Klaus Kandt, amesema huenda kuna mhalifu hatari katika eneo hilo na amewahimiza watu wawe chonjo.

Maafisa wanalichunguza lori lililotumiwa kufanyia shambulizi hilo kutafuta ushahidi wa vinasaba. Wanachunguza pia data za mfumo wa GPS wa lori hilo pamoja na taarifa kwenye simu za mkononi zilizopatikana katika eneo la tukio.

Polisi wa Berlin walisema wameshapokea taarifa karibu 500 kuhusu shambulizi hilo. Andrea Schulz, mwenyekiti wa chama cha maafisa wa ujasusi Ujerumani amekiambia kituo cha televisheni cha ZDF jana jioni kwamba wana matumai makubwa watafaulu na kuna nafasi nzuri watafanikiwa haraka kumkamata mshukiwa mpya.

Meya wa jiji la Berlin Michaal Müller alisema leo ni vizuri kuona wakaazi wa Berlin hawajatishika na haoni haja ya watu kuogopa. Müller aidha alisema maafisa zaidi wa polisi wametumwa kupiga doria na hatua zaidi za usalama zimeshachukuliwa.

Mwandishi:Josephat Charo/apa/reuters/dpa

Mhariri:Iddi Sessanga