Polisi waanzisha msako Mogadishu
15 Aprili 2013Afisa mkuu wa polisi nchini Somalia, Mohammed Hassan, amesema kwa sasa watu zaidi ya 400 wamekamatwa katika oparesheni hiyo ambayo inanuia kuimarisha usalama.
Jana Jumapili watu tisa waliokuwa wamevalia mikanda ya mabomu walijiripua katika majengo ya mahakama nchini humo, huku wengine wakifyatua risasi kiholela na kusababisha mauaji ya watu zaidi ya 30 huku wengine 20 wakijeruhiwa.
Mohammed Hassan amesema magari yote yanayoelekea mjini yanakaguliwa na abiria kuzuiliwa na kuhojiwa.
Wanajeshi wa Afrika wanaolinda amani nchini Somalia wameweka vizuizi vya barabarani kote mjini Mogadishu na wanafanya msako wa nyumba kwa nyumba kutafuta washukiwa wa kundi hilo la kigaidi.
Ali Ismail mkaazi wa Mogadishu amesema ameshuhudia watu takriban 300 wakizuiliwa na polisi huku wengine wakiwa wamefungwa vitambaa usoni.
Naye Yusuf Ganey ambaye pia ni mkaazi wa eneo hilo amesema hii sio oparesheni ya kawaida kwa kuwa polisi wanakamata mtu yeyote atakayeonekana barabarani.
Al Shabaab wakubali kuhusika
Kundi la al-Shabaab linaloaminika kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaida lilikubali kuhusika na mashambulizi hayo.
Kundi hilo lilikuwa linamiliki sehemu kubwa ya pwani ya Somalia hadi lilipotimuliwa mwaka wa 2011, na kwa sasa linaendelea na mashambulizi ya kiholela dhidi ya serikali inayoungwa mkono na jamii ya Kimataifa.
Hata hivyo shambulizi lililofanyika hapo jana katika majengo ya mahakama ambako usalama huwa umeimarishwa bado jambo hilo linawashangaza wengi, kwa kuwa hakuna mtu aliyedhani kwamba kundi hilo la al shabaab linaweza kutekeleza shambulizi kama hilo mahali ambapo serikali huendeshwa.
William Hague alaani shambulizi
Huku hayo yakiarifiwa Uingereza kupitia waziri wake wa mambo ya nchi za nje William Hague imesema kundi la kigaidi lililohusika na shambulizi hilo linaendelea kuyumbisha amani ya nchi hiyo na kuendeleza mateso kwa raia wa Somalia.
Katika taarifa yake Hague amesema amelaani vikali tukio hilo na kwamba waliohusika ni lazima wawajibishwe.
Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza amesema nchi yake pamoja na jamii ya Kimataifa bado imejizatiti katika kuwasaidia raia wa Somalia kupata amani, usalama na maendeleo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef