Polisi wa Zimbabwe waweka vizuizi vya barabarani
19 Januari 2019Msako huo ambao umekuwa unafanywa na majeshi ya usalama umeshutumiwa vikali na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binadamu na imetoa madai juu ya watu kupigwa risasi, kupigwa na kutekwa nyara kwa viongozi wa upinzani, wanaharakati na wananchi wa kawaida.
Mkakati wa kuweka vizuizi barabarani ulikuwa unatumiwa sana wakati wa utawala wa rais Robert Mugabe. Hata hivyo tabia hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa tangu Mugabe aondolewe madarakani na wanajeshi mnamo mwezi Novemba mwaka 2017 na nafasi yake kuchukuliwa na makamu wake Emmerson Mnangagwa.
Msemaji wa polisi Charity Charamba ameliambia gazeti la serikali,"Herald" kwamba polisi inataka kuwaambia wananchi kuwa vituo vya udhibiti wa usalama vimeshawekwa na polisi na kwamba idara nyingine za usalama zitakuwa zinafanya ukaguzi. Msemaji huyo ameeleza kuwa lengo la kuweka vizuizi hivyo ni kuwanasa wale wanaotuhumiwa kupora mali za watu. Amesema lengo ni kuzirejesha mali zilizoibiwa wakati wa maandamano.
Maandamano hayo yaliripuka baada ya rais Mnangagwa kutangaza ongezeko la bei ya mafuta ya petroli kwa asilimia 150 mwishoni mwa wiki iliyopita. Gazeti la "Herald" limeripoti kwaba watu 700 walikamatwa baada ya ghasia kuzuka na gazeti hilo limekitupia lawama chama cha upinzani cha MDC na vyama vya wafanyakazi kwa maandamano hayo.
Maripota wa shirika la habari la AFP wameshuhudia vizuizi hivyo vikifanya kazi katika mji mkuu Harare na katika mji wa Bulawayo ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Zimbabwe. Maripota hao walishuhudia jinsi polisi waliokuwa na bunduki walivyowasimamisha watu na kuwapekua kwenye vizuizi hivyo vilivyowekwa katika njia muhimu.
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa maandamano jumatatu iliyopita watu katika miji hiyo walijaribu kwenda madukani ili kujipatia mahitaji kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu. Watu walijipanga kwenye foleni ndefu ili kununua mikate na petroli bidhaa ambazo zimeadimika kutokana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaoikabili Zimbabwe lakini mtu mmoja amesema hakuna kilichobadilika tangu kuongezwa bei ya petroli.
Mitandao ya kijamii imefungiwa na serikali katika kile kinachoonekana kuwa njama za serikali hiyo za kuzuia habari juu ya hatua za kiusalama zinachokuliwa na polisi na pia kuzuia habari juu ya kukiukwa haki za binadamu.
Asasi ya kutetea haki za binadamu nchini Zimbabwe imesema imeorodhesha vifo vya watu wapatao 12 na watu wengine wapatao 78 wana majeraha ya risasi. Asasi hiyo pia imeripoti juu ya kadhia zaidi ya 240 ambapo watu walishambuliwa na kuteswa.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binadamu imeitaka serikali ya Zimbabwe iache msako inaoufanya na pia imeelezea wasiwasi juu ya matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na majeshi ya usalama. Kulingana na taarifa ya ofisi hiyo, polisi wametumia risasi za moto. Umoja wa Mataifa pia umetoa wito kwa serikali ya Zimbabwe juu ya kutafuta njia za kufanya mdahalo na wananchi ili kuyasikiliza malalamiko yao halali.
Wakati huo huo watumishi wa umma wamelikataa pendekezo la pili la serikali juu ya kuwaongezea mishahara na wametaka kulipwa kwa dola za Marekani. Wananchi wa Zimbabwe ambao sasa wamepungukiwa uwezo wa kununua mahitaji yao kutokana na mfumuko mkubwa wa bei, licha ya sarafu ya dola kuanza kutumika mnamo mwaka 2009, wamesema rais Mnangagwa bado hajatekeleza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za uchaguzi juu ya kuustawisha uchumi wa nchi baada ya Mugabe kuondoka madarakani.
Serikali ya Zimbabwe imependekeza kuongeza mishahara ya hadi dola 109 kwa mwezi lakini wafanyakazi wamelikataa pendekezo hilo. Naibu Mwenyekiti wa baraza linalojumuisha vyama vya watumishi wa umma bwana Thomas Mzondo amesema mazungumzo mengine na serkali yanatarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFP/RTRE
Mhariri: Sylvia Mwehozi