1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wawili wa Kosovo watiwa mbaroni Ujerumani

Isaac Gamba
23 Desemba 2016

 Wakati mshukiwa wa shambulizi la lori katika soko la Krismasi mjini Berlin raia wa Tunisia Anis Amri akiendelea kusakwa polisi  wanasema wamewatia mbaroni raia wawili wa Kosovo wakihusishwa na shambulizi la kigaidi.

https://p.dw.com/p/2UlqQ
Deutschland Anti-Terror-Einsatz im Centro Oberhausen
Picha: picture-alliance/dpa/A. Stoffel

Maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia sare za jeshi hilo na wale ambao walikuwa katika mavazi ya kawaida wakiwa na silaha waliwatia mbaroni watu wawili baada ya kuvamia eneo la maduka la Oberhausen na kufanya msako katika eneo hilo lililoko  katika  jimbo la North Rhine- Westphalia

Kwa mujibu wa taarifa za kipolisi  wanaume hao wawili  ambao ni ndugu wazaliwa wa Kosovo wenye umri wa miaka 28 na 31 wanashukiwa kutaka kufanya shambulizi katika eneo hilo la maduka  ikiwa ni pamoja na eneo maalumu la soko la Krismasi lililoko  kwenye maduka hayo. 

Maafisa wa usalama  nchini Ujerumani wanasema walifanya msako katika maeneo kadhaa mjini Berlin na katika maeneo mengine  kwa lengo la kumtia mbaroni  Anis Amri mwenye umri wa miaka 24 anayehusishwa na shambulizi la lori mjini Berlin lililoua watu 12 katika soko la Krisimasi mjini Berlin Jumatatu wiki hii.

 Amri anadaiwa kufikia katika eneo lililoko katika jimbo la North Rhine- Westphalia   wakati alipokuwa akitafuta hifadhi ya kuishi nchini Ujerumani katikati ya mwaka 2015.

Kansela Angela Merkel aonyesha matumaini ya kukamatwa haraka mshukiwa wa shambulizil la Berlin

Berlin PK zu LKW Anschlag Merkel, Maas, de Maiziere
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere Picha: Reuters/H. Hanschke

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ana matumaini ya kukamatwa haraka mshukiwa huyo na kuongeza kuwa ametiwa moyo na jinsi watu wengi nchini ujerumani walivyoonekana kuguswa na shambulizi hilo.

Gazeti moja la nchini Ujerumani la "Bild" limeripoti hii leo kuwa watu watatu miongoni mwa 12 waliouawa katika shambulizi hilo bado hawajatambuliwa.

Waliotambuliwa ni raia sita wa ujerumani, raia mmoja wa Israel, raia mmoja wa Italia pamoja na  raia wa Poland ambaye ni dereva la lori hilo lililokuwa na shehena ya bidhaa zilozukuwa zikitarajiwa kupakuliwa nchini Ujerumani.

Ama kwa upande mwingine maafisa wa usalama nchini Ujerumani wanasema walifanya msako katika basi lililokuwa limebeba watalii katika mji wa Heilbronn katika jimbo la kusini  la Baden- Wurttemberg. hata hivyo maafisa hao wanasema hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na msako uliofanywa kwenye basi hilo.

Mikanda ya vidio ya tangu jumatatu iliyopita ambayo taarifa zake zimechapishwa na vyombo kadhaa vya habari nchini Ujerumani inaonyesha kuwa  mshukiwa wa shambulizi hilo Anis Amri alitoweka mara tu baada ya kulibamiza lori hilo katika soko  la Krismasi mjini Berlin.

Chombo cha habari cha matangazo cha umma cha RBB cha mjini Berlin  kimeripoti kuwa picha zilimuonesha mshukiwa huyo saa chache baada ya shambulizi hilo akiwa katika eneo la msikiti  katika mji wa Moabit, eneo ambalo ndipo lori hilo lilipotekwa na baadaye kuuawa  dereva aliyekuwa akiliendesha.

Berlin Anschlag - Fahndungsfoto Anis Amri
Anis Amri mshukiwa wa shambulizi katika soko la Krismasi mjini BerlinPicha: picture-alliance/Bundeskriminalamt

Wakati huohuo kikosi maalumu cha polisi mjini Berlin kilivamia eneo linalodaiwa kutumiwa na wafuasi wa makundi ya itikadi kali ambalo inadaiwa kuwa mshukiwa Amri aliwahi kulitembelea.

Ama kwa upande mwingine waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere akizungumza baada ya kutembelea taasisi inayohusika na masuala ya uchunguzi nchini Ujerumani amesema alama za vidole zilizogunduliwa katika

 lori na ushahidi mwingine uliokwishapatikana unaonyesha kuwa mshukiwa wa shambulizi hilo anaweza kuwa ndiye mhusika mkuu wa mipango ya shambulizi hilo la jumatatu.

Aidha taarifa zinazohusiana na mshukiwa huyo Anis Amri kuwa miongoni mwa orodha ya ujerumani tangu mwezi  septemba ya watu wanaodhaniwa kuwa hatari zinazidi kuibua maswali juu ya hatua zinazochukuliwa na idara ya polisi nchini Ujerumani.

Mwandishi: Isaac Gamba/ DW/ipj/jm (dpa, Reuters, rbb)

Mhariri     : Daniel Gakuba