Polisi Ugiriki wadhibiti mripuko kwenye kifurushi
5 Novemba 2010Polisi nchini Ugiriki wamefanikiwa kudhibiti mripuko katika kifurushi kilichokuwa na bomu ambacho kilitumwa kwenda katika ubalozi wa Ufaransa mjini Athens.
Pia polisi hao waligundua vifurushi vingine kadhaa walivyokuwa wakivitilia shaka katika kampuni ya mizigo kwenye kitongoji kimoja cha mji huo.
Vifurushi hivyo vimepatikana siku chache baada ya vifurushi vingine vya mabomu kutumwa katika ofisi za balozi kadhaa na viongozi wa Ulaya, akiwemo Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.
Vifurushi 14 vya mabomu vilipatikana katika wiki iliyopita. Watu wawili wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi lenye msimamo mkali nchini Ugiriki wamekamatwa wakihusishwa na mabomu hayo.
Wakati huo huo, wizara ya ndani nchini Ufaransa imesema kuwa kifurushi kimoja cha bomu ambacho kilizuiliwa nchini Uingereza kikitokea Yemen kwenda Marekani wiki iliyopita, kilikuwa kiripuke dakika 17 tu kabla ya kuzuiwa.