Polisi Namibia wakamata mzigo unaoshukiwa kuwa na bomu
18 Novemba 2010Ofisi ya Uhalifu ya Shirikisho nchini Ujerumani-BKA, imesema kuwa sanduku lililoshukiwa kuwa na bomu ambalo lilipakiwa katika ndege iliyokuwa inaelekea nchini Ujerumani, limezuiwa nchini Namibia. Taarifa hiyo imetolewa leo, siku moja baada ya Ujerumani kuimarisha usalama kutokana na kuwepo hatari ya kutokea mashambulio ya kigaidi nchini humo.
Ofisi ya Uhalifu ya Shirikisho nchini Ujerumani-BKA, imesema mzigo uliokuwa unatiliwa shaka ulikamatwa jana katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Windhoek, Namibia kabla ya kupakizwa katika ndege ya shirika la ndege la Air Berlin iliyokuwa inaelekea Munich.
Katika taarifa yake, BKA, imeeleza kuwa uchunguzi ulibaini kwamba kifaa kilichokuwemo katika mzigo huo kilikuwa betrii iliyounganishwa na waya na saa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi unaoendelea utabaini iwapo kifaa hicho kilikuwa ni cha kuripuka. Abiria wote waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walikaguliwa tena na mizigo yao pamoja na ndege yenyewe kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari yake na waliwasili salama Munich jana usiku.
Ofisi ya BKA imesema kuwa imewapeleka maafisa wake Afrika Kusini wakiwa njiani kuelekea Namibia kusaidia kufanya uchunguzi na inapanga kupeleka wataalamu zaidi kuchunguza kifaa hicho kinachoshukiwa kuwa ni bomu. Akizungumza kutoka Pretoria Afrika Kusini, Henri Boshoff wa taasisi ya mafunzo ya kiusalama alisema, ''Tunachokiona hapa na nimeshatumia viwanja vingi hivi vya ndege ni mfumo wa kawaida ambao umewekwa na viongozi. Unakaguliwa, lakini mashirika mengi ya ndege ya kimataifa yanaweka usalama zaidi, yanatumia kampuni za usalama na kuna ukaguzi wa mwisho kabla ya kuingia ndani ya ndege.''
Serikali ya Ujerumani imeimarisha usalama katika vituo vya treni, viwanja vya ndege na maeneo ya wazi kutokana na kupatiwa taarifa na mshirika wake wa kigeni za uwezekano wa kufanyika mashambulio ya kigaidi yaliyopangwa mwezi huu. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere amesema kuwa tangu katikati ya mwaka huu vikosi vya usalama vinazidi kupokea taarifa kwamba mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda unataka kufanya mashambulio nchini Marekani, Ulaya na nchini Ujerumani.
Likinukuu duru za usalama, gazeti la Tagesspiegel limeripoti hii leo kwamba Marekani imeiambia Ujerumani kuwa kati ya mashambulio mawili au manne huenda yakafanywa na Al-Qaeda nchini Ujerumani na Uingereza. Miongoni mwa maeneo ya Ujerumani yanayolengwa ni katika soko la Krismasi. Mwezi uliopita polisi waligundua vifurushi viwili vilivyokuwa na mabomu vikitokea Yemen kuelekea Marekani, huku kifurushi kimoja kikiwa kimepitia katika uwanja wa ndege wa Cologne.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhan