1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi kutoa taarifa za kina kuhusu mashambulizi ya Cologne

Caro Robi11 Januari 2016

Maafisa wa Ujerumani wanatarajiwa kuwasilisha taarifa ya kwanza ya kina ya uchunguzi wao kuhusu mashambulizi yaliyotokea mjini Cologne mkesha wa mwaka mpya, ambapo wanawake walidhalilishwa kingono.

https://p.dw.com/p/1HbAV
Picha: Reuters/W.Rattay

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la North Rhine Westphalia Ralf Jaeger anatarajiwa kuwasilisha taarifa kuhusu mashambulizi hayo wakati atakapokuwa anahojiwa na wabunge wa jimbo hilo kuhusu matukio ya kudhalilishwa kwa wanawake, hali ambayo imemfanya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kumulikwa darubini kutokana na sera yake ya kuwapokea maelfu ya wakimbizi na wahamiaji Ujerumani.

Licha ya kuwa hakuna mashitaka rasmi yaliyofunguliwa dhidi ya washukiwa wa mashambulizi hayo ya Cologne, polisi imesema wengi wa washukiwa hao ni watu wanaotafuta hifadhi na wahamiaji haramu kutoka Kaskazini mwa Afrika.

Udhalilishaji huo ulichochea maandamano makubwa Cologne mwishoni mwa juma. Vuguvugu linalopinga wahamiaji Ujerumani la PEGIDA linatarajiwa kufanya maandamano mengine baadaye leo katika mji wa mashariki ya Ujerumani wa Leipzig.

Merkel ashutumiwa

Merkel amechukua msimamo mkali baada ya kisa hicho cha Cologne kwa kusema wakimbizi na wahamiaji wanaohusika katika uhalifu Ujerumani huenda wakanyimwa hifadhi na kurejeshwa haraka katika nchi zao.

Waandamanaji wa vuguvugu la PEGIDA wakikabilina na polisi Cologne
Waandamanaji wa vuguvugu la PEGIDA wakikabilina na polisi ColognePicha: Reuters/I.Fassbender

Maafisa wa chama chake cha kihafidhina wanatarajiwa wiki hii kujadili pendekezo la kubadilisha sheria kuhusu uhamiaji ili kuwarejesha haraka wanaokutikana na makosa ya uhalifu na uvinjifu mwingine wa sheria.

Merkel ameshutumiwa hata na wanachama wa chama chake kwa kuruhusu wahamiaji na wakimbizi kuingia kwa maelfu nchini humu. Wakosoaji wake wanahoji iwapo wakimbizi hao, wengi wao kutokea Syria, Iraq na Afghanistan wataweza kutangamana katika jamii.

Kabla ya mashambulizi hayo, Kansela huyo wa Ujerumani alishikilia msimamo wake kuwa ni jambo jema kuwakaribisha wahamiaji Ujerumani na barani Ulaya kwa jumla, lakini tangu mashambulizi hayo ameonekena kubadili sera ya kuwa mkarimu kwa wageni.

Waziri wa sheria wa Ujerumani Heiko Maas amesema anaamini mashambulizi hayo ya Cologne yalipangwa, mtizamo ambao pia umeelezewa na waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere

Polisi imesema hapo jana kuwa wamepokea malalamiko 516 kuhusu mashambulizi hayo ya mkesha wa mwaka mpya, zaidi ya wiki moja tangu yalipotokea na kuongeza asilimia 40 ya malalamiko hayo, yanahusiana na udhalilishaji wa kingono vikiwemo visa viwili vya ubakaji.

Walioshuhudia mashambulizi hayo wameelezea matukio ya kushtusha ambapo wanawake walitomaswa, kutukanwa na kuporwa na genge la vijana.

Ukubwa wa mashambulizi hayo umelishtua taifa la Ujerumani na kupelekea kurunzi kuelekezwa kwa wahamiaji zaidi ya milioni moja walioingia nchini humu mwaka jana.

Kura ya maoni iliyochapishwa na gazeti la Bild imeonyesha asilimia 39 ya wajerumani wanahisi polisi haikutoa ulinzi wa kutosha, huku asilimia 57 wakihisi polisi ilitoa ulinzi wa kutosha.

Je wageni ni kitisho Ujerumani?

Asilimia 49 ya wajerumani nao wanahisi genge hilo lililowadhalilisha wanawake huenda likaishambulia miji yao. Kichwa cha gazeti hilo jana lilikuwa swali la je matokeo ya kashfa ya mkesha wa mwaka mpya ni matokeo ya sera mbovu?

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/F.von Erichsen

Kura nyingine ya maoni iliyofanywa na shirika la habari la RTL liligundua kuwa asilimia 57 ya wajerumani wanahofia viwango vya uhalifu vitaongezeka kutokana na ongezeko kubwa la wahamiaji huku asilimi 40 wakipinga dhana hiyo.

Likinukuu ripoti za polisi ambazo hajizatolewa hadharani, gazeti la Bild am Sonntag limesema baadhi ya vijana kutoka kaskazini mwa Afrika walitumiana jumbe katika mitandao ya kijamii kuhimiza kukusanyika Cologne mkesha wa mwaka mpya.

Kwingineko, polisi mjini Hamburg wamesema wamepokea malalamiko 133 ya visa kama hivyo vya uhalifu katika mkesha wa mwaka mpya.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga