Polisi Hong Kong wapambana na waandamanaji
27 Mei 2020Hii inafuatia hatua ya serikali kuu ya China kuwasilisha pendekezo la sheria mpya ya usalama wa taifa na kuyarejesha maandamano hayo ya kuipinga serikali.
Katika wakati ambapo wasiwasi unazidi kuongezeka, polisi wa kukabiliana na waandamanaji walimwagwa katika eneo linalozunguka baraza la bunge la jijini Hong Kong, na kuwazuia waandamanaji waliopanga kukusanyika eneo hilo wakati muswada huo ukiwa njiani kujadiliwa na ambao utalifanya kosa la jina kuudharau wimbo wa taifa wa China.
Maduka mengi, mabenki na majengo ya ofisi yalifungwa mapema na polisi walionekana kuwazingira baadhi ya waandamanaji, na kuwalazimisha kukaa chini, pembezoni mwa barabara na baadae kuwapekua.
Maandamano haya ya karibuni kabisa kwenye jiji la Hong Kong yanafuatia pendekezo la serikali ya China wiki iliyopita kuelekea sheria ya usalama wa taifa linalolenga kukabiliana na kujitenga na shughuli za kigaidi katika jiji hilo. Sheria hizo zinazoependekezwa huenda pia zikapelekea idara za kijasusi za China kujikita jijini humo.
Marekani, Australia, Uingereza, Canada na mataifa mengine tayari yameelezea wasiwasi wao kuhusu sheria hiyo, inayoonekana na wengi kuwa ni hatua inayoweza kuubadilisha kabisa mji huo wa China ulio na uhuru mkubwa zaidi na moja ya vitovu vya kifedha duniani.
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye tayari yuko katika mzozo wa kibiashara na Beijing pamoja na janga la virusi vya corona, amesema jana kwamba Marekani wiki hii itatoa majibu mazito kuhusiana na sheria hiyo iliyopendekezwa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian ameng'aka mbele ya mkutano na waandishi wa habari akisema hawatakubali uingiliaji wa nje kwenye mambo ya ndani ya taifa hilo.
Alisema, "Suala la sheria ya usalama wa taifa katika jiji la Hong Kong ni suala la ndani kabisa la China. Hatutavumilia uingiliaji wowote wa nje. Tutachukua hatua muhimu za kupambana dhidi ya hatua zozote mbaya za uingiliaji wa kigeni huko Hong."
Mamlaka za China na serikali ya Hong Kong inayoungwa mkono na Beijing wanasema hakuna kitisho chochote kuelekea uhuru wa juu kabisa wa jiji hilo la Hong Kong.
Katibu mkuu wa Hong Kong Matthew Cheung alinukuliwa akisema sheria hiyo indhamiria kuleta utulivu wa muda mrefu kwa Hong Kong na China, na haitaathiri uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni na haitaathiri hadhi ya jiji hilo kama kitovu cha kibiashara. Aliongeza kuwa itawezesha mazingira thabiti ya biashara.
Soma Zaidi: Idara za usalama Hong Kong zaonya kitisho cha ugaidi
Mashirika: AFPE/RTRE