Poland yasisitiza itaendelea na uchimbaji makaa ya mawe
5 Desemba 2018Mwenyeji wa mkutano huo Poland inashinikiza kupatiwa ulinzi utakaoiruhusu kuendelea kuchimba nishati hiyo ya makaa ya mawe. Wakati mataifa yakiwa kwenye mazungumzo ya Umoja wa Mataifa ya mabadiliko ya tabia nchi yenye lengo la kuzuwia ongezeko la ujoto duniani, sehemu nyingi duniani tayari zinakabiliwa na vimbunga, mafuriko, mikasa ya moto na ukame ambao huathiri dunia. Uzalishaji wa gesi ya ukaa umeongezeka kwa mwaka tangu kufikiwa kwa makubaliano ya Paris 2015, na maendeleo ya kisiasa yakisuasua, watu watakaobeba mzigo mzito wamepaza kilio chao sasa kukomeshwa uchimbaji wa nishati ardhini.
Mpango wa matakwa ya wananchi umetiwa saini na watu karibu 300,000 kutoka Zaidi ya nchi 120. Unazitaka nchi tajiri ambazo zinawajibika sana kuzalisha gesi ya ukaa, kuheshimu ahadi zao kuyafadhili mataifa yaliyoko hatarini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na uchumi ulioendelea kuwa kijani kufikia mwaka 2030.
Mnamo mwezi Oktoba, jopo la wataalamu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa, lilitoa matokeo ya wazi kabisaa juu ya gesi ya ukaa, na kupendekeza kupunguzwa kwa nusu, gesi chafu zinazotokana na mafuta ya kuchimbwa ardhini katika kipindi cha miaka 12 ijayo, ili kufikia lengo la makubaliano ya Paris la kupunguza joto duniani. Lakini mataifa mengi ya magharibi yangali yanategemea uzalishaji wa mafuta ya kuchimbwa.
Poland ambayo hupata karibu asilimia 80 ya umeme wake kutoka makaa ya mawe, wiki hii iliyataka mataifa kubuni hatua ndani ya mfumo wa Tabianchi wa Umoja wa Mataifa, ambao wakosaoji wanahofu utairuhusu kuendeleza uchafuzi kwa miongo kadhaa.
Rais Andrzej Duda alitumia hotuba yake wakati wa sherehe za ufunguzi wa COP 24 siku ya Jumatatu kusema utegemezi wa Poland katika makaa ya mawe, haulingani na ulinzi wa mazingira na maendeleo yaliopatikana kwenye mzunguko huo. Duda alisisitiza ujumbe wake tena siku ya Jumanne wakati alipozungumza na wachimbaji kwenye mji wa kusini akisema hatoruhusu mtu yeyote kuua sekta ya uchimbaji ya Poland.
Poland na nchi nyingine zinazotegemea uchimbaji mafuta zinasema wanahitaji kipindi cha mpito kuelekea nishati itakayowalinda wachimbaji na usalama wa nishati ya nchi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, aliwaambia maafisa kwenye majadiliano siku ya Jumanne kwamba "mjadala na viwanda wakati mwingine ni mgumu'.
Nchi zilizotia saini makubaliano ya Paris zilikubaliana kupunguza ongezeko la joto duniani chini ya nyuzi 2 na hadi nyuzi 1.5 kwenye kipimo cha Selshiasi. Lakini Umoja wa Mataifa ulionya mwezi uliopita kwamba pengo kati ya gesi ya ukaa na kiwango kinachohitajika kufikia lengo la makubaliano ya Paris ni kikubwa kuliko hapo awali.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga