Poland yaota kufanya makubwa Uefa, Euro 2012
8 Juni 2012Poland wenyeji wenza wa mashindano haya wana ndoto za kupata mafanikio makubwa na sio tu kwasababu wao ni wenyeji, pamoja na kwamba jukumu hilo linatoa hamasa kubwa. Lakini enzi za mafanikio makubwa ya soka kwa Poland zimepita, ambapo mafanikio pekee makubwa ni katika mwaka 1974 na 1982 , ambapo nchi hiyo ilishika nafasi ya tatu katika fainali za kombe la dunia.
Poland katika miaka ya hivi karibuni ilidorora na kuyaaga mashindano ya fainali za kombe la dunia na kombe la mataifa ya Ulaya katika duru za mwanzo.
Kocha Franciszek Smuda ana kibarua kigumu mbele yake. Kundi hili la A linatimu zinazolingana kiuwezo, lakini hii haina maana ya kuondoa hamasa kwa Poland. Kocha Smuda anawategemea sana wachezaji wake nyota wa mabingwa mara mbili nchini Ujerumani na mabingwa wa kombe la shirikisho, DFB Pokal , Borussia Dortmund. Jakub , Kuba , Blaszcykowski, Lukasz Piszczek na mshambuliaji Robert Lewandowski ni nyota wanaong'ara nchini Poland.
Hii itakuwa historia kubwa kwa nchi yetu, amesema mlinzi wa Borussia Dortmund na Poland, Lukasz Piszczek, akiwa na furaha kubwa. Nahodha Kuba Blaszcykowski anatoa lengo la timu yake kuwa ni kufika robo fainali kwanza. Kabla ya hapo, lakini, kuna kibarua dhidi ya Ugiriki hapo Ijumaa Juni 8 mjini Warsaw wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo.
Huu ndio mchezo muhimu sana kwetu. Kabla ya mashindano haya ya Euro 2012, kulikuwa na hali ya wasi wasi kutokana na kashfa ya rushwa pamoja na utata dhidi ya mlinzi Piszczek katika kashfa ya kupanga matokeo katika kikosi hicho cha Poland. Smuda pamoja na hayo amemuita mlinzi huyo katika kikosi hicho na kumtupa nje ya kikosi Slawomir Peszko kutoka FC Köln kutokana na kashfa ya ulevi.
Katika orodha ya timu bora duniani, Urusi imo katika nafasi ya 11 na ni timu inayoonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuvuka kiunzi hicho cha makundi, na kufuatiwa na Ugiriki iliyo katika nafasi ya 14 katika orodha ya timu bora duniani. Lakini Urusi kukosa kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2010 kuliwahuzunisha sana. Wakati huo kikosi cha kocha Guus Hiddink kilikwama katika michezo ya awali ya kufuzu kucheza fainali hizo na kocha huyo alifungishwa virago na kurejea kwao Uholanzi. Matarajio kwa mrithi wa kiti cha Hiddink, Dick Advocaat, ni makubwa. Lakini hata hivyo Advocaat yuko njiani kukiacha mkono kikosi hicho cha Urusi kwani anarejea nyumbani baada ya mashindano haya, tayari kushika usukani wa kukiongoza kikosi cha timu ya daraja la kwanza nchini Uholanzi ya PSV Eindhoven.
Advocaat amekiongoza kikosi cha Urusi kupitia nahodha Andrej Arschavin na mshambuliaji Pavel Pogrebnjak, katika awamu ya kufuzu kucheza fainali hizi na ana matumaini , kwamba ukosoaji dhidi ya timu hiyo ya taifa utakuwa umepitwa na wakati.
Ugiriki, chini ya kocha wao Mjerumani, Otto Rehhagel , ilitawazwa mabingwa wa Ulaya mwaka 2004, lakini tangu wakati huo kikosi hicho hakijaonyesha makali yake ya hapo zamani. Fernando Manuel Costa Santos anatafuta mbinu za Rehhagel za ukuta pamoja na wachezaji wakongwe , kama Theofanis Gekas, kuleta mafanikio katika timu hiyo. Kocha huyo wa taifa la Ugiriki anaweza kupata mafanikio , kupitia nyayo alizopitia mtangulizi wake Otto Rehhagel.
Jamhuri ya Czech iliwahi kuvuma. Majina yaliyobaki katika kumbukumbu ni kama Pavel Nedved na Karel Poborsky, lakini pia bado wapo mlinda mlango wa Chelsea London, Petr Cech, na Tomas Rosicky wa Arsenal London. Mwaka 1976 iliyokuwa Yugoslavia ya zamani ilitawazwa mabingwa wa kombe la Ulaya na mwaka 2004 Jamhuri ya Czech iliyokuwa sehemu ya Yugoslavia , ilifikia nusu fainali ya kombe la Euro. Tangu wakati huo jamhuri ya Czech imekuwa katika nafasi za kati kwa kati. Lakini sasa kocha Michal Bilik ameibadilisha sana timu hiyo, kwa kuwapa nafasi vijana wengi chipukizi na ana matumaini kuwa kikosi hicho kitanusurika katika duru hii ya makundi.
Mwandishi : Olivia Fritz / ZR/ Sekione Kitojo
Mhariri : Othman Miraji.