1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland yaadhimisha karne moja ya kuanzishwa Jamhuri ya pili

11 Novemba 2018

Usalama umeimarishwa kwenye mji mkuu wa Poland, Warsaw kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanyika na viongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia kusherehekea karne nzima tokea nchi hiyo kupata uhuru.

https://p.dw.com/p/382o3
Polen | Warschau verbietet Nationalistenmarsch am Unabhängigkeitstag
Picha: Reuters/Agenzia Gazeta

Kila Novemba 11 Poland inaadhimisha kuanzishwa kwa Jamhuri ya pili ya Kipolishi mnamo mwaka 1918 katika eneo ambalo lilichukuliwa na majirani zake wa mashariki na magharibi katika karne ya 18, hatua hiyo iliwezekana baada ya kushindwa kwa Urusi, Ujerumani na Austria katika Vita Vikuu vya Kwanza.

Mwaka jana, maandamano hayo ya Novemba 11 yanayoandaliwa na viongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia yaligubikwa na ubaguzi huku waandamanaji wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa "damu safi, akili safi" na Ulaya itabaki kuwa ya watu weupe.

Maandamano hayo yanaweka wazi mjadala kuhusu kama chama cha kihafidhina cha Sheria na Haki – PiS cha serikali kinayahimiza makundi yenye mizizi katika mavuguvugu ya kifashisti na yanayopinga baadhi ya jamii za asili ya kigeni.

Kauli hizo zimeibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa hisia za chuki dhidi ya wageni katika wakati ambao nchi nyingine za Ulaya pia zinapambana na kufufuka kwa hisia kali ya mrengo wa kulia.

"Kinachotuleta pamoja ni bendera ya Poland ya rangi nyeupe na nyekundu,” Waziri wa Mambo ya Ndani Mariusz Blaszczak ameiambia televisheni ya taifa TVP. "Nnamkaribisha kila mmoja kuhudhuria”.

Chama cha PiS kinasema kinapinga ubaguzi lakini wakosoaji wanakituhumu kwa kuegemea kisiri upande wa mrengo wa kulia.

Tangu kilipochaguliwa 2015, chama hicho kimeifanya Poland kuendelea kutengwa Ulaya wakati kukiwa na tuhuma kuwa kinaelekea katika utawala wa kimabavu. 

Ubalozi wa Marekani mjini Warsaw ulitoa tahadhari ya usalama kabla ya maandamano hayo. Wizara ya Ulinzi ya Poland imesema msafara wa kijeshi yakiwemo magari ya kivita utaandamana na matembezi hayo, lakini ikasema kuwa hawako sehemu y mipango yoyote ya usalama.

Pia leo Jumapili, viongozi wa dunia wanakusanyika Paris kuadhimisha kumalizika kwa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid