1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Platini amkosoa Blatter, amuunga mkono Mwanamfalme Ali

25 Mei 2015

Rais wa UEFA Michel Platini ametangaza kumuunga mkono Mwanamfalme wa Jordan Ali bin al Hussein katika jitihada zake za kumwondoa usukani Sepp Blatter kama mkuu wa shirikisho la kandanda ulimwenguni FIFA

https://p.dw.com/p/1FWFB
Österreich Michel Platini beim UEFA-Kongress in Wien
Picha: Reuters/L. Foeger

Katika mahojiano yaliyochapishwa leo na gazeti la L'Equipe, Platini amesema Blatter alimdangaya miaka minne iliyopita aliposema kuwa muhula wake wa sasa wa nne ungekuwa wake wa mwisho. Anasema Blatter hataki kusalia uongozini kwa sababu ana kazi ya kumalizia au kwa sababu ana miradi kadhaa mikubwa anayotaka kuifanya kwa niaba ya FIFA, bali anahofia hatma yake maishani kwa sababu maisha yake yote yamekuwa katika FIFA.

Platini anaamini sasa ni wakati muafaka wa uongozi mpya katika shirikisho hilo na kuwa Mwanafalme Ali ndiye mtu anayefaa kupewa wadhifa huo. Mwanafalme Ali ndiye mgombea pekee aliyesalia kupambana na Blatter katika uchaguzi wa urais wa FIFA, ambao utafanyika Ijumaa hii mjini Zurich, baada ya kujiondoa Mreno Luis Figo na Mholanzi Michael van Praag.

Mwanamfalme Ali, mwenye umri wa miaka 39 na mwanachama wa kamati kuu ya FIFA, anazingatiwa kuwa mgombea mwenye maendeleo na manifesto yake imejikita sana katika suala la kuwepo uwazi katika shirkisho la kandanda ulimwenguni.

Rais wa Shirikisho la kandanda la Uholanzi Van Praag aliahidi kumuunga mkono Mwanamfalme Ali, akisema njia pekee ya kumwondoa Blatter usukani ni kwa wapinzani kuungana.

UEFA, ambao ina kura 53 kati ya 209 zitakazopigwa, imesema haitamuunga mkono Blatter, lakini Mswisi huyo ameahidiwa kuungwa mkono na mashirikisho mengi ya kandanda ulimwenguni.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu