1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PKK yadai kuchukua miili ya wanajeshi wawili wa Uturuki

Kalyango Siraj6 Oktoba 2008

Uturuki yawalaumu wa Kurdi wa Iraq kwa kusaidia PKK

https://p.dw.com/p/FUmR
Malori ya kijeshi ya Uturuki katika harakati dhidi ya waasi wa Kikurdi wa PKKPicha: picture-alliance/ dpa

Kundi la waasi wa Kikurdi la Kurdistan Workers' Party PKK limedai kuwa na miili ya wanajeshi wawili wa Uturuki waliouawa katika hujuma za waasi hao dhidi ya vituo vya kijeshi karibu na mpaka wa Uturuki na Iraq.Nalo jeshi la Uturuki kwa upande wake linawalaumu wakurdi wa Iraq kwa kuwasaidia, kwa hali na mali, waasi wa Kikurdi wa Uturuki.

Madai ya waasi yametolewa leo jumatatu kufuatia mapigano ya mwishoni mwa juma yaliyotokea kusini mashariki mwa Uturuki ambapo,kwa mujibu wa jeshi la Uturuki, wanajeshi 15 waliuawa na wengine wawili kutojulikana waliko.

Kupitia taarifa, kundi la PKK limesema kuwa kitengo chake cha kijeshi maarufu kama,jeshi la watu wa Kurdistan,lilichukua miili ya wanajeshi wawili wa Uturuki baada ya mapigano yaliyotokea katika maeneo ya Shamzinyan.

Kundi hilo linadai kuwa waasi waliwauwa wanajeshi 62 na kuwajeruhi wengine 23. Aidha taarifa hiyo pia imedai kuwa waliidengua ndege ya kijeshi ya Uturuki aina ya Helikopta na pia kuteka silaha nyingi.

Jeshi la Uturuki, kwa upande wake, linakiri kuwa wanajeshi wake 15 walifariki katika shambulio la waasi hao na pia nalo likawauwa waasi takriban 23.

Jana jumapili waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan,alitoa ombi kwa wakurdi wa Iraq kuchukua hatua muafaka dhidi ya PKK,ikisemekana kuwa wapiganaji hao wamejificha katika milima ya kaskazini mwa Iraq.

Waziri mkuu huyo alikuwa katika mazishi ya mmoja wa wanajeshi waliouawa na waasi wa PKK katika mashambulio ya mwishoni mwa juma.Akiwa katika kijiji cha Armutlu karibu na mji wa Ankara, kwenye mazishi yalihudhuriwa na watu karibu 2,000,amesema kuwa hatua madhubuti zitachukuliwa dhidi ya PKK hasa kuhusu maficho yao.

Serikali ya Ankara inadai kuwa waasi wa PKK hupata silaha kirahisi nchini Iraq na kuzitumia kufanya mashambulizi ndani mwa Uturuki.

Watawala wa Iraq wamekuwa wakitoa ahadi za kukabiliana dhidi ya waasi wa PKK lakini inasema kuwa maficho yao yako milimani jambo ambalo,wanasema , linatatiza shughuli za kuwakabili. Nae rais wa utawala wa Kikurdi nchini Iraq ,Massud Barzani,amelaani mashambulio ya mwishoni mwa juma na kusema kuwa hayasaidii yeyote anaetaka kuleta amani na utulivu katika eneo hilo.

Waziri mkuu wa Uturuki baada ya mazishi jana alisema kuwa maafisa wandamizi,watakutana alhamisi kujadili hatua zaidi dhidi ya waasi hao.Alikuwa akitamka hayo huku waombolezaji wakipaza sauti wakipinga kundi hilo la PKK.

Na katika maeneo ya kusini mashariki mwa Uturuki, jeshi limekuwa linazidisha wanajeshi pamoja na vifaa vya kijeshi karibu na maeneo ya mpaka na Iraq.Ndege za helikopta zilikuwa zikiruka kupita maeneo ambapo waasi walipitia na pia mizinga zaidi iliyalenga maeneo ya milima inayoinamia mpaka wa Uturuki na Iraq.

Kundi la PKK limeorodheshwa kama kundi la kigaidi, sio tu nchini Uturuki, lakini pia katika Umoja wa Ulaya, pamoja na Marekani.Limekuwa likipigania kujitawala ama uhuru wa ndani kwa eneo lenye wakurdi la Uturuki tangu miaka ya 1980.

Jeshi la Uturuki linasema kuwa takriban watu 35,000 wamekufa katika mapigano na waasi hao tangu yaanze.