Pistorius hakuwa na "matatizo ya kiakili"
30 Juni 2014Imewachukua siku 30 wataalamu hao wa masuala ya saikolojia na magonjwa ya akili kutoa ripoti hiyo ambayo ilitokana na uamuzi wa jaji Thekozile Masipa kutaka Oscar Pistorius kupimwa akili baada ya mwanariadha huyo kudai kuwa anakabiliwa na matatizo ya kupatwa na wasiwasi.
Mwendesha mashtaka wa serikali Genrrie Nel ambaye ndiye ambaye alisoma matokeo ya ripoti hiyo. Baada ya kusomwa kwa matokeo ya ripoti hiyo ya wataalamu wa magonjwa ya akili na saikolojia, yalifuata maelezo ya daktari Gerry Versveld ambaye ndiye aliyemfanyia operesheni ya miguu mwanariadha huyo.
Katika ushahidi wake Dr Versveld amesema maumivu na pamoja na hali ya kutokujiamini inayomkabili Postorius kutokana na kutumia kwake miguu ya bandia kunaweza kulichangia kumuongezea wasiwasi ambao ulisababisha kumuua kwa kumpiga risasi mpenzi wake.
Ilimbidi Dr Verseveld kutoa maelezo hayo baada ya mawakili wanaomtetea mwanaridha huyo kutaka kufanya hivyo ili adhihirishe kuwa miguu hiyo ya bandia ya Pistorius inachangia kumuongezea wasiwasi mwanariadha huyo.
Katika hatua nyingine Pistorius aliionesha mahakama jinsi anavyovua miguu yake hiyo ya bandia, mwendesha mashtaka wa serikali Nel alimuuliza Dr Verseveld kama Pistorius anaweza akasota katika giza bila ya kuanguka ili kupata ukweli wa madai ya mwanariadha huyo kwamba hakumuona mpenzi wake wakati alipokuwa anaenda bafuni, Dr Verseveld alijibu swali hilo kwa kusema inategemea na kutanda kwa giza katika nyumba.
Oscar pistorius alioekana ni mtulivu wakati wote ripoti hiyo ilipokuwa inasomwa mahakamani pamoja na ushahidi mwingine, kesi hiyo imeahirishwa mpaka pale jaji Masipa atakapotoa hukumu ambapo endapo kama mwanariadha huyo atapatikana na hatia ya mauaji ya kukusudia anaweza akafungwa kifungo cha maisha.
Mwandishi: Anuary Mkama/afpe, dpae
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman