Pillay alaani ghasia Syria
14 Februari 2012Saa chache baada ya Mkuu huyo wa kamisheni ya kutetea haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay kuwahutubia wanachama wa Umoja huo mjini New York Marekani, vikosi vya Syria viliendeleza mashambulizi zaidi dhidi ya waandamanaji katika mji wa Homs na kuifanya siku hii kuwa siku ya 10 tangu serikali hiyo kuanzisha vurugu dhidi ya Upinzani katika eneo hilo.
Pillay amesema kufuatia hatua ya Urusi na China kutumia kura ya turufu kupinga maazimio ya Umoja wa Mataifa, yaliomtaka Rais Bashar Al Assad aondoke madarakani, Serikali ya Syria imepata nguvu zaidi ya kuwakandamiza raia wake kwa kutekeleza uhalifu dhidi ya binadamu.
Pillay amesema kwa sasa ripoti zinaonyesha zaidi ya watu 5,400 waliuwawa mwaka jana huku idadi hiyo ya waliofariki pamoja na waliojeruhiwa ikipanda kila siku.
Kulingana na ripoti yake, mwishoni mwa mwezi January vikosi vya serikali vimewaua zaidi ya watoto 400, huku watoto watoto chini ya miaka 10 wakinyanyaswa na kufungwa pamoja na watu wazima huku wakinyimwa chakula na maji.
Kutokana na hilo wanadiplomasia katika mkutano huo mkuu wa Umoja wa Mataifa wamesema mswada wa azimio linalounga mkono mpango wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu kutuma vikosi vya kulinda amani nchini Syria ikijumuisha pia vile vya Umoja huo huenda ukapigiwa kura baadaye wiki hii.
Mkuu wa kikao hicho cha Umoja wa Mataifa wa Qatar Nassir Abdulaziz al-Nasser amesema hali nchini Syria haishikiki tena. Al Nasser amesema nchi za Kiarabu zinaandaa muswaada mpya utakaosambazwa pia katika nchi jirani kwenye eneo hilo leo au kesho. Muswaada huenda ukapigiwa kura wiki hii.
Aidha ripoti ya Navy Pillay imesema jeshi la Syria sasa, limepitisha sera ya kupiga risasi na kuuwa. Mkuu huyo wa kamisheni ya kutetea haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa ameonesha wasi wasi na masikitiko yake kufuatia visa vya dhulma za kimapenzi hasaa ulawiti wa wanaume na watoto wa kiume katika jela nchini humo.
Huku hayo yakiarifiwa mkuu wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu Nabil al-Arabi yuko Ujerumani kufanya mazungumzo juu ya Syria na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Mwandishi Amina Abubakar/RTRE
Mhariri Yusuf Saumu