Pik Botha wajihi wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini afariki
12 Oktoba 2018Botha amefariki dunia leo alfajiri akiwa nyumbani kwake baada ya kuuguwa kwa muda mfupi, amesema mwanawe wa kiume Roelf Botha mbele ya maripota wa kituo cha matangazo cha Afrika Kusini eNCA news.
Kimataifa Pik Botha alikuwa mwakilishi bayana wa mfumo wa ubaguzi wa rangi na mtengano-apartheid, katika wakati ambao utawala huo ulikuwa ukizongwa na malalamiko na vikwazo vya kimataifa, malalamiko yaliyomalizikia kwa kuchaguliwa Nelson Mandela kuwa rais wa kwanza mweusi mwaka 1994.
Alitetea hatua za serikali yake kila mahala ingawa alitambua baadae umuhimu wa mageuzi. Aliwashangaza walimwengu na hasa rais wa Afrika Kusini wakati ule P.W. Botha aliposema mwaka 1986 Afrika Kusini inaweza siku moja kuongozwa na mtu mweusi.
"Mustakbali wa Afrika Kusini utaakuwa mwema waafrika na wazungu wakiungana" anasema Pik Botha
"Tunabidi tufanikiwe. Ulimwengu unataka tufanikiwe. Katika wakati ambapo enzi za ubaguzi wa rangi na mtengano apartheid zinatoweka kitakuwa kiroja kikubwa na balaa kama wa-Afrika Kusini watashindwa kujongokeana na kukubaliana kusonga mbele na kuigeuza nchi yao iwe ya kidemokrasi, kama tulivyostahiki kuwa na kupata sifa ambazo nchi yetu inazostahiki."
Pik Botha ambae hatokani na ukoo mmoja na rais wa zamani wa Afrika Kusini P.W. Botha, aliteuliwa kuwa waziri wa maadini na nishati katika serikali ya Nelson Mandela na kusema mwaka 2000 angependelea kujiunga na chama cha African National Congress ANC-chama tawala kilichoendesha mapambano kwa miongo kadhaa dhidi ya utawala wa wazungu wachache.
Pik Botha amefurahishwa na kukabidhiwa Cyril Ramaphosa hatamu za uongozi wa Afrika Kusini
Lakini kuanzia wakati ule Pik Botha alikuwa tayari ameanza kujitenga na siasa. Matamshi yake ya mwisho aliyoyatoa miaka ya hivi karibuni yalihusiana na kashfa iliyomkaba rais wa zamani Jacob Zuma aliyejiuzulu february iliyopita."Botha alifurahi sana aliposikia Cyril Ramaphosa amekabidhiwa nafasib ya Zuma, alisikia Pik Botha akisema. Itafaa kusema Pik Botha aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje kati ya mwaka 1977 hadi mfumo wa aparthheid ulipokoma mwaka 1994, alihusika na mazungumzo mwishoni mwa miaka ya 80 yaliyopelekea Namibia kupata uhuru .
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/AP/Reuters
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman