Picha za waandishi wa habari wa Kiafrika
Mwaka huu, tuzo ya ya umma ya haki za binadamu Afrika, inayotolewa na DW chini ya tuzo ya vyombo vya habari Ujerumani kwa sera za maendeleo, imewaangazia wapiga picha wa Kiafrika. Hizi ni baadhi ya picha bora zaidi.
Haki ya kupata elimu
Watoto hawa kutoka Makoko wako njiani kurudi nyumbani wakitokea shule. Eneo la mabanda limejengwa juu ya nguzo ndani ya wangwa wa Lagos. Elimu ni silaha bora zaidi dhidi ya umaskini. Lakini katika eneo la mabanda la Makoko, ambalo ni miongoni mwa maeneo yenye umaskini mkubwa zaidi Lagos, watoto wengi hawana nafasi ya kwenda shule. Hawa wamebahatika.
Matumizi ya nguvu ya polisi
Mwendesha pikipiki mjini Lagos anasihi asamehewe. Aliamua kuvua nguo zote kama ishara ya kupinga kukamatwa kwake. Mwaka 2012 utawala wa Lagos ulikataza usafiri wa pikipiki kuendeshwa katika barabara kuu. Polisi imelaumiwa kwa sababu inatumia nguvu na vitisho kusimamia sheria hiyo mpya.
Haki ya kutoa habari
Waandishi wa habari wa Kisomali wanaandamana kupinga kukamatwa na kuuwawa kwa wenzao. Katika tukio hili alikuwa amekamatwa mwandishi wa habari mmoja aliyekuwa amemhoji mwanamke aliyebakwa. Mwaka 2012 waandishi wa habari 18 waliuwawa Somalia. Nchi hiyo ni miongoni mwa nchi hatari zaidi kwa waandishi.
Unyanyasaji wa kijinsia
Akiwa na umri wa miaka 87, Nikiwe Masango kutoka Jambeni, Afrika Kusini, alikuwa mhanga wa unyanyasaji wa kijinsia. Anakumbuka kwamba alizinduka usingizini usiku na kukuta mwanamme mmoja amemlalia juu. "Nadhani alikuwa amenipulizia dawa ya usingizi kwa sababu sikusikia chochote," anasema. Alibakwa usiku mzima. "Alinilazimisha nifunge macho ili nisiweze kumtambua."
Hamu
Raia huyu wa Afrika Kusini alikuwa jela kwa miaka 20. Kila tatoo katika uso wake inaonyesha nafasi yake katika kundi la wahalifu. Picha hii inaonyesha kuwa kila mtu ana uzuri wake, haijalishi yuko katika hali gani ya kimaisha.
Uzazi salama
Zeituni anaona fahari kumbeba mtoto wake mchanga. Mama na mtoto wana afya njema. Zeituni alikwenda katika hospitali iliyo karibu na nyumbani kwake kujifungua. Hospitali hiyo iko katika kijiji cha Diff, kwenye eneo la mpaka kati ya Kenya na Somalia. Wodi mpya ya uzazi iliyopo hapo ni wodi pekee ya aina hiyo katika eneo zima.
Kuchukua sheria mikononi
Mwanamme huyu anaburuzwa katika mitaa ya Cape Town. Kabla ya hapo alipigwa na watu kwa sababu inasemekana alikuwa ameiba simu. Baadaye mtu huyo alipelekwa hospitalini lakini hakuna aliyekamatwa kwa sababu ya kile alichofanyiwa. Hapa, haki ya kuendeshwa kwa kesi yenye usawa ilikanyagwa kwa miguu.
Kufukuzwa
Mwanamke huyu yuko barabarani na analia mbele ya watoto wake saba. Yeye na familia yake walitolewa kwa nguvu katika nyumba yao kwenye mji mkuu wa Chad, N'Djamena. Katika eneo hilo itajengwa hoteli ya kifahari. Zaidi ya watu 670 walifukuzwa na nyumba zao kubomolewa. Hakuna aliyelipwa fidia.
Adhabu ya kupigwa
Maafisa wa kulinda usalama wanambeba mwanaharakati Boniface Mwangi kutoka Kenya. Katika mkutano mmoja wa hadhara, alikuwa amesema kwa nguvu kuwa mwanachama mmoja wa chama cha wafanyakazi alikuwa "msaliti". Mwangi alipigwa na kuwekwa mahabusu. Hii ni kwa sababu tu alitumia uhuru wake wa kutoa maoni.
Uhaba wa maji
Wakaazi hawa wa kijiji cha Jatokrom, kaskazini mwa Ghana, wametembea umbali wa kilometa nyingi kupata maji katika bwawa hili. Mto uliopo karibu na mashamba yao umekauka. Bwawa hili linatumika pia kunywesha wanyama ni hivyo maji yake hayafai kwa binadamu kunywa. Mpaka leo, mamilioni ya Waghana hawana huduma ya maji safi ya kunywa.
Huduma duni ya vyoo
Mvulana huyu anaruka msururu wa vibanda vya vyoo huko Khayelitsha, karibu na Cape Town, Afrika Kusini. Kwa watu waishio katika maeneo ya mabanda kuzunguka Cape Town, ni shida sana kwenda chooni. Vyoo vya umma vimejaa, ni vichafu na havifanyiwi ukarabati. Kwa sababu ya kuogopa wahalifu, watu wengi huamua kutumia ndoo badala ya kwenda chooni.