Petraeus- Machafuko Afghanistan kuendelea
10 Desemba 2009Afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani ameonya ufanisi wa kijeshi nchini Afghanistan, utachukua muda mrefu kuliko ilivyokuwa nchini Iraq, licha ya kuongezwa kwa idadi ya wanajeshi nchini humo. Akitoa ushahidi mbele ya baraza la Congress Generali David Petraeus, alisema kama ilivyokuwa Iraq, hali nchini Afghanistan itazidi kuwa mbaya, kabla ya kuimarika.
Generali Petraeus alikuwa anazungumza wiki moja baada ya Rais Barack Obama kuagiza kupelekwa kwa wanajeshi elfu 30 zaidi nchini Afghanistan. Kulingana na mkakati wa Obama, wanajeshi wote elfu 30, wanatarajiwa kuwa wamewasili nchini Afghanistan mwaka ujao, kujaribu kukabiliana na vita vya miaka minane dhidi ya Taliban, na kutoa nafasi majeshi ya Marekani kuanza kuondoka ifikapo Julai mwaka wa 2011.