Peru inaongoza kwa kasi kubwa ya vifo vya Covid-19
1 Juni 2021Serikali ya Peru imesema imeongeza idadi ya vifo kutoka 69,342 hadi 180,764 kufuatia ushauri wa jopo la wataalamu wa afya, lililogundua kulikuwepo na mapungufu katika kuhesabu. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la AFP, kufuatia usahihishaji huo, Peru sasa inaongoza kwa kuwa na kasi kubwa kabisa ya vifo vilivyosababisha na virusi vya corona kuliko nchi yoyote duniani, ikiwa na vifo 5,484 katika kila wakazi milioni moja.
Kwa mujibu wa data za AFP, Peru, yenye wakazi milioni 33 awali iliorodheshwa katika nafasi ya 13 duniani ikiwa na vifo 2,103 kwa kila watu milioni moja. Peru imeorodhesha zaidi ya maambukizi milioni 1.9 hadi leo, na katika siku za hivi karibuni imekabiliwa na uhaba mkubwa wa gesi ya oksejeni kuwatibu wagonjwa wa corona.
Waziri Mkuu wa Peru, Violeta Bermudez amesema idadi ya vifo ilisahihishwa kufuatia ushauri wa jopokazi lililopendekeza marekebisho ya mfumo wa kuweka data wa Peru.
"Mojawapo ya changamoto za janga hili imekuwa kuweka rekodi ya watu waliokufa katika daftari, kwa kuwa mienendo ya iana mpya ya virusi ilihitaji mbinu maalumu, miundombinu na itifaki ambazo sio kila taasisi ilikuwa imeandaliwa kuzishughulikia".
Jopo hilo lilisema katika ripoti yake kuwa mfumo uliopo ulitoa matokeo yasiyo sahihi yalioonesha idadi ndogo ya vifo kutokana na ugonjwa wa COVID-19.
Majina mapya ya aina za virusi vya corona
Wakati haya yakiarifiwa shirika la afya duniani WHO limetangaza mfumo mpya wa kuzipa majina aina mbalimbali za virusi vya corona kutumia alfabeti ya Kigiriki. Aina hizo awali zilikuwa na majina kutegemea na herufi na nambari au nchi zilikogunduliwa kwanza. Shirika hilo limesema linatumai kuleta uwiano katika usawa na uelewa juu ya aina za virusi vya corona zinazotia wasiwasi, kwa kutumia mfumo huo mpya.
Kwa mantiki hiyo aina ya kwanza ya virusi hatari vilivogunduliwa nchini Uingereza vinavyojulikana kama B1.1.7 sasa vitaitwa "alpha". Aina ya pili iliyogunduliwa nchini Afrika Kusini ambayo imejulikana kama B 1.351 sasa itaitwa "beta". Na aina ya tatu iliyopatikana nchini Brazil itaiwa "gamma" na ya nne iliyogunduliwa India itajulikana kwa jina la delta. Aina mpya hatari za virusi vya corona zitakazogunduliwa siku za usoni zitapewa majina kutumia alfabeti ya Kigiriki.
WHO imesema kundi la wataalamdu walipendekeza mfumo huo mpya ambao hautachukua mahala pa mifumo ya kisayansi ya utoaji majina, lakini utatoa njia rahisi ya kutamka na kuyakumbuka majina ya aina za virusi vya corona. Soma zaidi Afrika Kusini yarejesha vizuizi vikali vya Covid-19
Hapa nchini Ujerumani hatua zilizowekwa kuzuia kuenea kwa virusi vya corona huenda zikafika mwisho ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema hayo jana akidokeza kuwa zinaweza kurejeshwa iwapo kutajitokeza aina mpya ya virusi, kitu ambacho wanatumai hakitatokea. Merkel amesema hatua za kudhibiti corona zimechangia sana juhudi za kudhibiti wimbi la tatu la maambukizi na amewashukuru Wajerumani kwa kujitolea kwao katika miezi iliyopita, akisisitizha kuwa changamoto ya corona bado ipo.