"Penye mabomu watu wanakufa bila hatia"
5 Oktoba 2015Gazeti la "Thüringer Allgemeine" linasema vifo vya madaktari na wagonjwa 22 katika hospitali ya Kunduz vilikuwa vya kikatili na havikuwa na sababu. "Ni kama vile walitaka kuthibitisha kuwa dhana ya kwamba kuna vita vya haki ni uongo mtupu," anasema mhariri wa gazeti hilo na kukumbusha kuwa mahali popote yanaporushwa mabomu lazima pawe na watu wanaokufa bila hatia - iwe mashambulizi ya anga yanayofanywa na Wamarekani mjini Kunduz ama mashambulizi ya anga Syria yanayoendeshwa na majeshi ya serikali, Marekani na washirika wake na pia Urusi, ambapo ripoti za vifo vya raia wa kawaida zinapuuzwa kama propaganda.
Kwa upande wake, gazeti la "Freie Presse" la mjini Chemnitz linaangalia chanzo cha machafuko mjini Kunduz. Vikosi vya NATO vilipoondoka Afghanistan mwishoni mwa mwaka 2014, wataalamu wengi wa masuala ya jeshi walionya kwamba hatua hii imekuja mapema mno. Na kweli, wanamgambo wa Taliban baada ya mfupi walifanikiwa kutawala maeneo kadhaa. Hata hivyo, kuongeza muda wa maaskari wa kigeni kukaa Afghanistan pia kusingesaidia. Wataalamu na mawaziri wa ulinzi wa mataifa ya NATO watakapokutana hivi karibuni wanapaswa wabuni mpango utakaoiletea Afghanistan mustakabali wenye amani.
Wakimbizi watakiwa kuheshimu sheria
Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linabaini kuwa wiki nne baada ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kutamka kwa imani kubwa "Tutaweza," akizungumia changamoto ya kukabili wakimbizi, wale wanaojitolea kuwahudumia wahamiaji wanasikika wakiguna, "Hatutaweza kuendelea kwa muda mrefu." Wasiwasi unaoletwa na msururu wa wakimbizi usiokoma unaambatana na habari zinazosikika kwenye kambi za kuwapokea wakimbizi. Mapigano wakati wa kugawa chakula, unyanyasaji wa kijinsia, kutishiwa kwa watu wenye dini ya tofauti. Ndio maana waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maizière amesisitiza kwamba wakimbizi lazima waelewe kuwa hakuna mjadala kuhusu kufuata sheria za msingi za Ujerumani, kama vile uhuru wa dini, haki sawa kati ya wanaume na wanawake na uhuru wa kutoa maoni.
Wakatoliki kulegeza sheria za ndoa?
Maaskofu wa kanisa katoliki wanakutana kwenye makao makuu ya kanisa hilo, Vatican, katika sinodi ya familia. Mkutano huo wa wiki tatu unajadili msimamo wa kanisa katoliki juu ya mambo yote yanayohusu familia. "Mada ya moto kabisa katika sinodi hii ni namna ambavyo kanisa litashughulikia watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja," anasema mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten." Sinodi inakutanisha makundi mawili yenye misimamo tofauti kabisa: Kwa wahafidhina, mashoga ni watu wenye dhambi wanaokwenda kinyume na Mungu na kinyume na misingi ya uumbaji. Kwa mtazamo wa wale wasio na msimamo mkali wa kidini, kanisa halina haki ya kuwa mlinzi anayeamua nani anayeruhusiwa kuingia kwenye nyumba ya ibada na yupi haruhusiwi kuingia, kwa sababu ametenda dhambi.
Nalo "Nürnberger Nachrichten" linasema: Papa Francis ameweka wazi kuwa kanisa lazima liwe nyumbani kwa watu ambao hawafuati mafundisho ya dini kikamilifu. Papa anawachukulia watu kuwa sehemu ya kanisa, hata kama wametoka kwenye ndoa iliyovunjwa kwa talaka au kama ni mashoga. Kwa upande mwingine, labda Papa Francis amewavunja moyo wale waliodhani kwamba ataleta mageuzi makubwa katika suala hili.
Mwandishi: Elizabeth Shoo
Mhariri: Josephat Charo