Pendekezo la wakurd kuhusu kura ya maoni ya uhuru lakataliwa
25 Oktoba 2017Serikali ya Iraq mjini Baghdad haikulijibu bado pendekezo hilo. Hata hivyo msemaji wa vikosi vya Haj al Chabi, vinavyowasaidia wanajeshi wa serikali katika mapambano yao dhidi ya wafuasi wa itikadi kali wa Dola la Kiislam - IS, na dhidi ya wanamgambo wa kikurdi wa Peshmerga, amelikataa moja kwa moja pendekezo hilo.
Mwezi mmoja uliopita, jimbo hilo la kaskazini mwa Iraq linalojivunia utawala wa ndani, liliitisha kura ya maoni ambapo kura ya "ndio" iliibuka na ushindi mkubwa. Kura hiyo ya maoni ya kudai uhuru ikawa chanzo cha kuripuka mzozo usiokuwa na kifani pamoja na viongozi wa mjini Baghdad wanaoungwa mkono na nchi jirani za Uturuki na Iran, zilizopania kwa upande wao kukomesha juhudi za muda mrefu za jamii ya wachache ya wakurdi kudai uhuru wao.
Matokeo ya kura ya maoni yabatilishwe, wanasema viongozi wa Baghdad
Wakijivunia uungaji mkono huo, lakini pia na msimamo wa Marekani na mataifa mengine ya dunia kupinga kura hiyo ya maoni, waziri mkuu wa Iraq Haider al Abadi akatuma wanajeshi katika eneo hilo la kaskazini. Vikosi hivyo havijakawia kuyateka maeneo yote yaliyokuwa yakidhibitiwa na wanamgambo wa Peshmerga nchini Iraq. Sharti pekee la kuepukana na harakati hizo za kijeshi, ni kubatilisha matokeo ya kura hiyo ya maoni, wamesema viongozi wa serikali ya mjini Baghdad ikiwa ni pamoja na rais Fouad Massdoum ambae binafsi ni wa kabila la Kurd.
Hadi wakati huu lakini viongozi wa jimbo la Kurdistan la Iraq walikataa masharti yoyote kufungamanishwa na mazungumzo pamoja na viongozi wa mjini Baghdad. Lakini jana, mapigano yakazuka tena kati ya wanamgambo wa kikurdi na wanajesjhi wa Iraq katika eneo linalopakana na Uturuki na viongozi wa Baghdad wanaonyesha wamepania kuvidhiiti vituo vyote na njia zote muhimu kuelekea jimbo hilo la kaskazini.
Pendekezo la wakurdi lakataliwa na wanamgambo wa Haj Ahmed al Assad
"Ili kuepukana na balaa la vita na maaangamizi, viongozi wa Erbil wamependekeza kwa hivyo kusitisha matokeo ya kura ya maoni ya uhuru na kuanzisha mazungumzo pamoja na viongozi wa Baghdad kuambatana na katiba. Taarifa iliyotangazwa leo alfajiri inasema pia kwamba viongozi wa mjini Erbil wako tayari kuweka chini silaha mara moja. Pendekezo hilo halina maana yoyote, amesema msemaji wa wanamgambo wa Haj Ahmed al Assad. "Kusitisha" inamaanisha wanaendelea kuyatambua matokeo ya kura ya maoni, serikali ya Iraq lakini inataka, "yabatilishwe moja kwa moja".
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/AFP/Reuters
Mhariri: Gakuba, Daniel