1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pendekezo la EU kutaka mjumbe kwa Afghanistan lapitishwa

8 Oktoba 2021

Umoja wa Ulaya umefanikiwa katika juhudi za kutaka Umoja wa Mataifa umteuwe mjumbe mpya maalumu kwa  Afghanistan, pamoja na uwepo wa upinzani mkali kutoka kwa mataifa kama China, Urusi na Pakistan.

https://p.dw.com/p/41R3D
Pictures of the Week in the Middle East Photo Gallery
Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Mjumbe huyo atakuwa na wajibu wa kufuatilia hali ya upatikanaji haki katika taifa hilo, baada ya kuingia katika udhibiti wa Taliban, na atapaswa kutoa mapendekezo ya kufanywa maboresho ya ustawi wa haki. Balozi wa Umoja wa Ulaya katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Lotte Knudsen, amesema uteuzi wa mjumbe huyo ni muhimu katika kuzuia hali kuwa mbaya zaidi nchini Afghanistan.

Ameiita hatua hiyo kuwa ni muhimu katika hakikisho la kuendelea na uangalizi dhidi ya hali ilivyo nchini humo, kwa kupitia mtaalamu huru, na kadhalikia kudhibiti hali kuwa mbaya zaidi.

Balozi huyo amesema haki za wasichana na wanawake ni kipaumbele, kwa sababu vitendo vya Taliban vinakiuka haki za makundi hayo. Miongoni mwa mataifa 47 wanachama wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, 28 zimeunga mkono pendekezo hilo la Umoja wa Ulaya, 14 zimejizuia kupiga kura, huku tano tu: China, Urusi, Pakistan, Venezuela na Eritrea zikilipinga.

Urusi kuwa mwenyeji wa mkutano wa Taliban.

Afganistan, Flughafen in Kabul
Ulinzi katika uwanja wa ndege wa KabulPicha: Wakil Kohsar/AFP/Getty Images

Katika hatua nyingine, Urusi inajiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Taliban na makundi mengine yanayopingana nchini humo, katika mkutano uliopangwa kufanyika baadaye mwezi huu. Mwanadiplomasia mwandamizi wa Urusi, Zamir Kabulov, ambaye ni mjumbe wa taifa hilo kwa Afghanistan, amesema mkutano huo ambao utafanyika kwa muundo wa upatanishi wa Kirusi, unatarajiwa kufanyika Oktoba 20, ingawa hakusema ni nani hasa atakaliwakilisha kundi la Taliban katika mkutano huo.

Lakini pia taarifa ambazo zimetangazwa na mashirika ya habari ya Urusi zinasema wanadiplomasia wakiwemo wa Urusi, Marekani, China na Pakistan watafanya mazungumzo kuhusu Afghanistan mwezi huu.

Kwa muda mrefu, Urusi imekuwa ikifanya kazi ya kufanikisha mawasiliano mema na Afghanistan ingawa kwa namna rasmi taifa hilo linaichukulia Taliban kama kundi la kigaidi.

Chanzo: AP/AFP